FAO yapata fedha za kukabili nzige Kenya, Ethiopia na Somalia

24 Februari 2020

Wito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka wahisani kusaidia harakati za kukabiliana na nzige wavamizi wa jangwani huko Mashariki mwa Afrika umeanza kuitikiwa ambapo msaada wa karibuni zaidi ni wa dola milioni 10 kutoka taasisi ya Bill na Melinda Gates.

Msaada huo umewakilishwa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO ambapo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo lenye makao  yake mjini Roma, Italia, QU Dongyu amekaribisha na kutoa shukrani kwa taasisi hiyo.

Taarifa ya FAO iliyotolewa mjini Roma, Italia imesema kuwa fedha hizo, “zitasaidia serikali za Ethiopia, Kenya na Somalia katika kukabiliana na kuzaliana kwa nzige ambao wanatishia uzalishaji wa chakula na harakati za kujipatia kipato kwa wakazi wa ukanda huo.”

Bwana Qu ameshukuru taasisi hiyo na kusema kuwa, “nasihi wahisani wengine nao wafuate mfano wao ili tuweze kulinda njia za kipato za wakazi wa vijijini, kusaidia wakulima pia na familia zao.”

Baa la sasa la nzige ni baya zaidi kuwahi kukumba Ethiopia na Somalia katika kipindi cha miaka 25 na ni kiwango cha kuzaliana kwa nzige nchini Kenya ni kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 70.

Kwa mujibu wa jarida la FAO, Desert Locust Watch, Djibouti na Eritrea nazo pia zimeathirika na wimbi la nzige limeenea maeneo ya kusini mashariki mwa Sudan Kusini na Uganda hadi kusini magharibi mwa Iran.

Kwa sasa FAO imeongeza ombi lake la fedha hadi dola milioni 138 kutoka ombi la awali la dola milioni 76 lililotolewa mwezi mmoja uliopita kwa lengo la kusaidia nchi zilizoathirika.

Hadi sasa ni dola milioni 33 tu zilizokwishaahidiwa au kupatikana.

FAO
Utabiri wa FAO kuhusu mwelekeo wa nzige wa jangwani kwenye eneo la pembe ya Afrika kwa mwezi Machi hadi Juni 2020

Hali ya nzige wavamizi inatia shaka

Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO akizungumza hali ya sasa ya wadudu hao hatari amesema kuwa inatia wasiwasi mkubwa na kwamba wiki chache zijazo zitakuwa muhimu katika kuanzisha operesheni fanisi ya kudhibiti nzige hao wa jangwani.

“Ongezeko la wadudu hao linatishia vipato vya watu na usalama wa chakula kwenye eneo hilo ambalo tayari linakabiliwa na uhaba wa chakula.  Hakuna muda wa kupoteza,”  amesema Bwana Qu.

Nzige wa jangwani anatambuliwa kuwa mdudu wa kuhamahama hatari zaidi duniani na kundi dogo la wadudu hao lililopo kwenye usawa wa kilometa 1 ya mraba, linaweza kula chakula kinachotosheleza watu 35,000 kwa siku moja.

Wakiwa katika mazingira mazuri ya kuzaliana, wanataga mayai haraka na kuzaliana na idadi yao inaweza kuongezeka mara 500 katika kipindi cha miezi 6.

 

TAGS: Nzige, Bill na Melinda, FAO, QU Dongyu

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud