Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya mpito Sudan Kusini yaundwa, Guterres apongeza

Makubaliano ya kihistoria ya kuhuisha amani Sudani Kusini yatiwa saini kati ya rais Salva Kiir (kulia) na kiongozi wa upinzani Riek Machar, pichani ewakishikana mikono mjini Addis Ababa 12/9/2018
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Makubaliano ya kihistoria ya kuhuisha amani Sudani Kusini yatiwa saini kati ya rais Salva Kiir (kulia) na kiongozi wa upinzani Riek Machar, pichani ewakishikana mikono mjini Addis Ababa 12/9/2018

Serikali ya mpito Sudan Kusini yaundwa, Guterres apongeza

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha hatua ya kuundwa kwa serikali ya mpito ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, TGoNU, hii leo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani imemnukuu Katibu Mkuu akipongeza pande zote kwa hatua hiyo muhimu katika kutekeleza mkataba mpya wa amani uliotiwa saini mwaka 2018 huko Addis Ababa nchini Ethiopia mwaka 2018.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa hafla ya kuundwa kwa serikali hiyo imefanyika kwenye mji mkuu Juba huku Riek Machar akiapishwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais.

Rais Salva Kiir ameshuhudia tukio hilo lililofanyika Ikulu ambapo Bwana Machar ameripotiwa kusema kuwahakikishia wananchi wa Sudan Kusini kuwa atafanya kazi pamoja na wenzake ili kumaliza machungu ya wananchi wa Sudan Kusini.

Katibu Mkuu amepongeza pia hatua za kikanda na za kimataifa zilizochangia matokeo yaleo.

Ametoa wito kwa wanachama wa serikali hiyo ya mpito kuzingatia kwa nia njema barua na nia ya mkataba huo, ili wananchi wa Sudan Kusini waweze hatimaye kupata manufaa ya amani ya kudumu na utulivu ambavyo ni haki yao.

Amesema kwa upande wake Umoja wa Mataifa uko tayari kwa ushirikiano wa karibu na mamlaka ya kiserikali kwenye ukanda huo, IGAD pamoja na Muungano wa Afrika kusaidia pande husika katika kutekeleza mkataba huo.

Leo tarehe 22 mwezi Februari ilikuwa ndio tarehe ya mwisho kwa pande kinzani nchini Sudan Kusini ziwe zimeunda serikali hiyo ya Umoja wa kitaifa kama njia ya kutekeleza mkataba wa amani.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vilianza mwezi Desemba mwaka 2013.