Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaeleza hofu yake kubwa zaidi juu ya virusi vya Corona

Mfano wa virusi vya corona
Centers for Disease Control and Prevention
Mfano wa virusi vya corona

WHO yaeleza hofu yake kubwa zaidi juu ya virusi vya Corona

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema kuwa hofu yake kubwa zaidi hivi sasa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona, COVID-19 kuingia katika mataifa yenye mifumo dhaifu ya afya hususan barani Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo wakati akizungumza kwenye kikao cha dharura kati ya shirika lake na Kamisheni ya Afrika na kituo cha Afrika cha kudhibiti magonjwa, ACDC.

Akizungumza kwa njia ya video, Dkt. Tedros amewaeleza mawaziri wa afya wa Afrika kuwa ni kwa hofu hiyo ndio maana ofisi ya WHO Afrika kwa ushirikiano na ACDD wanafanya kazi kwa juhudi kubwa kuandaa mataifa ya Afrika pindipo virusi hivyo vinaingia.

Maandalizi hayo ni pamoja na uteuzi wa wajumbe maalum wawili ambao ni Dkt. John Nkengasong na Profesa Samba Sow ambao wana jukumu la kupatia nchi za Afrika ushauri wa kimkakati kuhusu virusi hivyo vya Corona na uchechemuzi wa ngazi ya juu kisiasa.

“Tumeandaa pia mpango mkakati wa maandalizi ambapo tumetoa ombi la dola milioni 675 za kusaidia nchi, hususan zile ambazo ziko hatarini zaidi,”  amesema Dkt, Tedros akiongeza kuwa tayari WHO imetambua mataifa 13 ya vipaumbele katika mkakati huo kutokana na uhusiano wa moja kwa moja na China na hata safari za kiwango kikubwa na taifa hilo la Asia ambako virusi hivyo vilianzia.

Grace Kaneiya
Fahamu kuhusu virusi vya corona na namna ya kujikinga

Amesema kuwa maandalizi hayo pia ni kusambaza vipimo vya uchunguzi wa virusi hivyo akisema kuwa hivi sasa idadi kubwa ya nchi za Afrika zina uwezo wa kupima COVID-10 kupitia vikasha vya mabara vilivyosambazwa na WHO, ikilinganishwa na wiki chache zilizopita.

Pamoja na kuimarisha uchunguzi kwenye maabara wamewasiliana na kampuni zinazotengeneza vifaa vya kujikinga wahudumu wa afya ili kuhakikisha kuwa nao wanalindwa.

Dkt. Tedros amezungumzia mafunzo kwa wahudumu wa afya akisema kuwa, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, wahudumu wafya 11,000 wa Afrika wamepata mafunzo kupitia kozi za mtandaoni za WHO kuhusu COVID-19, na mafunzo hayo yanapatikana bure  mtandaoni kwa lugha ya kiingereza, kifaransa na lugha zingine kupitia OpenWHO.org.

Shaka na Shuku

Wakati visa vya wagonjwa vikiripotiwa kupungua nchini China, Dkt. Tedros amesema fursa ya kukabili virusi hivyo inazidi kuwa finyu kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa nje ya China.

Hivi sasa China imeripoti kwa WHO wagonjwa 75,569 ambapo kati yao hao 2239 wamefariki dunia.

“Takwimu kutoka China zinaonesha kupungua kwa visa vipya. Hizi ni habari njema, lakini tunapaswa kutafsiri kwa umakini. Ni mapema mno kuwa na makadirio yoyote kwa mlipuko  huu. Nje ya China kuna wagonjwa 1220 katika mataifa 26 na vifo 8. Kama mjuavyo kuna kisa kimoja cha Corona kimethibitishwa barani Afrika huko Misri,”  amesema Dkt, Tedros.

Ameongeza kuwa nchi za kadhaa za Afrika zilikuwa na visa shukiwa vya Corona lakini kwa bahati nzuri vyote vimebainika si vya kweli.

Amesema ingawa idadi ya visa vinapungua China, bado wana hofu juu ya kukosekana kwa uhusiano wa dhahiri kama vile historia ya mgonjwa kusafiri kwenda China au mgonjwa kuwa na mahusiano au makaribiano na mgonjwa aliyethibitishwa.

 “Tunatoa wito kwa mataifa kuwekeza haraka kwenye kujiandaa. Tunapaswa kutumia fursa ya sasa tuliyo nayo ya kukabili virusi hivi kwa hali ya udharura,”  amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO.