Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wanaokimbia ukatili wapata kimbilio kupitia chifu mji wa Kaya, Burkina Faso

Familia waliokimbia machafuko wakiwa ndani ya chandarua kambi ya Pissila nchini Burkina Faso
WFP/Marwa Awad
Familia waliokimbia machafuko wakiwa ndani ya chandarua kambi ya Pissila nchini Burkina Faso

Wakimbizi wanaokimbia ukatili wapata kimbilio kupitia chifu mji wa Kaya, Burkina Faso

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati janga la kibinadamu likishuhudiwa nchini Burkina Faso, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema ongezeko katika mashambulizi linasababisha raia kukimbia kuelekea maeneo ya kusini karibu na Mali na Niger.

Katika mji wa Kaya nchini Burkina Faso wakimbizi wanaendelea kukimbia wakati huu ambapo, UNHCR inasema wakimbizi 765,000 ni wakimbizi wa ndani. 

Dianbendé Madiaga ni kiongozi wa jamii ambaye anasema tangu mtu wa kwanza alipowasili na kusema kwamba alikimbia kuokoa maisha na anahitaji makazi, alimkaribisha na tangu wakati huo watu wengi zaidi wamekimbia makazi yao kufuatia ukatili wa makundi yaliyojihami.“Kama chifu, ni wajibu wangu kuwapokea wale wanaokuja kusaka usaidizi.”

Rinata ni mmoja wa wakimbizi waliokaribishwa eneo la Kaya na anasema alishuhudia jamaa zake wakipigwa risasi. Lakini alifanikiwa kukimbia yeye na mume wake na wanae watano na Bwana Madaiga amewasaidia.“Ametusaidia kwa kutupatia chakula. Wake zake wametusaidia kwa kutupa vifaa vya kupikia kwa sababu wakati tuliondoka hatukuweza kuleta chochote. Anatusaidia hata na maji. Ni changamoto kubwa hapa. Hakuna maji.”

Familia ambazo Bwana Madiaga anasaidia ni kutoka makabila ya Mossi, Fulsé, Peul, Maransé, Gourmatché na Bella. 

Pia amekuwa akitoa msaada na ardhi yake ili watu wapate malazi huku akiomba pia majirani zake wafanye hivyo.

Rinata anasema msaada ambao ameupokea umemuwezesha kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wanawake wanaokabiliwa na kiwewe juu ya kubakwa au kuuawa kwa waume zao.

“Chifu na wake zake kweli wananisaidia. Wanazungumza nami. Na hicho kinanisaidia kutia moyo wanawake wengine na kuwaambia kwamba kuna watu hapa ambao wanaweza kuwasaidia.”

UNHCR imeweka makazi ya dharura kwa familia zilizo hatarini zaidi lakini kuna ukoseru wa maeneo salama zilizo na ulinzi  huku wengi wa watu waliokimbilia kaya wakilala nje kwenye baridi.