Wakati idadi ya maambukizi ya virusi vya corona COVID-19 ikiendelea kuongezeka kila uchao, Shirika la afya ulimwenguni, WHO limehimiza jamii ya kimataifa kuwekeza katika suluhu za afya ambazo zinaweza kusaidia katika kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo sasa na wakati huo huo kusaidia katika kujiandaa kwa ajili ya kuwekeza katika jamii kwa siku za usoni.
Wito huo umetolewa siku chache baada ya taarifa ya shirika la fedha duniani, IMF ya makadirio yake kuhusu athari za mlipuko wa virusi vya corona kiuchumi. Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva amesema ni muhimu kukumbuka kwamba,“Kuhusu hali ilivyo sasa, huenda hali tulio nayo sasa ni athari za muundo wa herufi V, kwa maana kuwa kutakuwa na kushuka kwa shughuli za kiuchumi nchini China ikifuatiwa na kuibuka kwa haraka na athari kwa China zikadhibitiwa. Kwa mantiki hiyo athari kwa uchumi wa dunia pia zitadhibitiwa.”
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu huyo amesema hali ya China na uchumi wa dunia kwa sasa ni tofauti kuliko ilivyokuwa wakati wa mlipuko wa homa ya mafua, SARS, “Uchumi wa China ni muhimu kwa dunia. Wakati huo ilikuwa asilimia 8 ya uchumi wa dunia. Sasa ni asilimia 19 na sasa ina uhusiano zaidi kwa Asia na dunia nzima. Kwa hiyo, tafrani huenda zikashuka chini na kufika hadi nchi zingine. Na tatu uchumi wa dunia katika miaka ya mwanzo wa 2,000 ulikuwa katika nafasi nzuri lakini leo tunakadiria ukuaji mdogo zaidi wa asilimia 3.3 kimataifa. Ni ukuaji mdogo baada ya kushuka katika kipindi cha mwaka mmoja. Kufuatia sababu hizo, ni lazima tufuatilie ni nini athari na kugeuza hali ya sasa kuwa makadirio.”
Kwa mujibu wa WHO idadi ya vifo kutokana na virusi vya corona nchini China Februari 21 saa kumi na mbili alfajiri saa za Geneva ni 2,239, visa 75, 567 vilivyothibitishwa na nje ya China idadi ya maambukizi ni visa 1,152 vilivyothibitishwa na vifo 8 katika nchi 26.