Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa heri Kakuma! Narejea Ethiopia lakini katu sitosahau Kenya- Mkimbizi

Pichani ya mtazamo kutoka angani inaonyesha sehemu ya makazi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya
Picha/Siegfried Modola
Pichani ya mtazamo kutoka angani inaonyesha sehemu ya makazi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya

Kwa heri Kakuma! Narejea Ethiopia lakini katu sitosahau Kenya- Mkimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kundi la wakimbizi 76 kutoka Ethiopia waliokuwa wanaishi kwenye kambi  ya Kakuma nchini Kenya wamerejea nyumbani ikiwa ni mara ya kwanza ya  utekelezaji wa mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari kwa wakimbizi hao wa Ethiopia. 

Kwenye kiwanja kidogo cha ndege huko Kakuma nchini Kenya, ndege hii inawasili tayari kurejesha nyumbani wakimbizi wa Ethiopia walioishi nchini Kenya, wengine hadi miaka 12 na hata kuzaliwa kwenye ardhi ya taifa hili la Afrika Mashariki.

Mpango huu unatekelezwa kwa pamoja na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR na serikali za Ethiopia na Kenya,ikiwa ni sehemu ya mwelekeo wa sasa wa maelfu ya raia wa Ethiopia wanaoishi kwenye ukanda huu kuchagua kurejea nyumbani kwa hiari kutokana na mabadiliko chanya nchini mwao.

Zaidi  ya nusu ya wanaotaka kurejea nyumbani ni wanawke na wasichana na miongoni mwao ni Faith Osman ambaye anasema kuwa, “nilifika hapa mwaka 2009. Nilikuwa mdogo. Sikufahamu kuandika wala kusoma na ndio maana nilikuja Kenya. Kenya imekuwa nzuri kwetu, kwa hiyo siwezi kusahau Kenya lakini narejea nyumbani.”

Safari ya ndege hii iliyokodishwa na UNHCR ilianza na kuelekea mji wa mashariki mwa Ethiopia wa Dire Dawa ambapo kutoka hapa raia hawa watasafiri kwa njia ya barabara hadi Jijiga, mji mkuu wa jimbo la Somali nchini Ethiopia.

Baada ya kuwasili, taratibu zinafanyika na UNHCR inawapatia misaada kadhaa ikiwemo mlo na fedha za kuwawezesha kufika makazi yao ya awali. Ann Encontre ni mwakilishi wa UNHCR nchini Ethiopia. Bi. Encontre anasema, “hii in haki ya msingi kwa wakimbizi wote kurejea nyumbani pindi wanapotaka kufanya hivyo. Wanarejea nyumbani na kuanzisha familia zao kule vijijini ambako walilazimika kukimbia na sisi UNHCR tuna furaha sana hii leo.”

Kurejea nyumbani kwa wananchi haw ani hatua ya kihistoria katika harakati za kusaka suluhu ya kudumu ya moja ya mizozo ya muda mrefu ya wakimbizi barani Afrika, kufuatia kurejea kwa wakimbizi wengine 94 wa Ethiopia kutoka nchini Sudan mwezi Juni mwaka 2019.

UNHCR inasema kuwa wakimbizi wengi zaidi wa Ethiopia walioko Kakuma na Daadab wanatarajiwa kurejea nyumbani katika miezi ijayo.

Hadi sasa zaidi ya wakimbizi 10,000 wa Ethiopia wanaoshi nchi jirani wameonyesha nia yao ya kurejea nyumbani kutoka Djibouti, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Yemen.