Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa UN washutumu adhabu ya kifungo kwa waandishi wa habari Burundi

Mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa David Kaye
UN /Jean-Marc Ferré
Mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa David Kaye

Wataalamu wa UN washutumu adhabu ya kifungo kwa waandishi wa habari Burundi

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameshutumu vikali adhabu ya kifungo cha miaka miwili na nusu jela dhidi ya waandishi wa  habari wanne walioandika habari kuhusu mapigano kati ya jeshi la nchi  hiyo na kikundi cha kigaidi cha Red-Tabara kaskazini mwa nchi hiyo.

Waandishi hao wa habari Christine Kamikazi, Agnès Ndirubusa, Térence Mpozenzi na Egide Harerimana,  ambao wanafanyia kazi chombo huru cha hababari cha Iwacu, walikamatwa tarehe 22 mwezi Oktoba mwaka jana wakiwa wanaelekea jimbo la Bubanza kuandika habari za mapigano.

Tarehe 30 mwezi uliopita wa Januari, Mahakama Kuu ya Burundi iliwahukumu kila mmoja kifungo cha miaka miwili na nusu jela na faini ya dola 530 kwa kosa la kutishia usalama wa taifa, kosa ambalo kwa mujibu wa ibara ya 16 ya kanuni ya makosa ya uhalifu ya Burundi ni kosa.

Wataalamu hao avid Kaye na Michel Forst, kupitia taarifa yao iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR,  wamesema, “baada ya kesi iliyogubikwa na kasoro nyingi, hukumu dhidi ya wanahabari hao waliokuwa wakifanya kazi yao haikubaliki. Waandishi wa habari wanapaswa kufanya kazi yao kwa uhuru na wapatiwe taarifa bila vikwazo vyovyote.”

Halikadhalika wamesema kuwa wanne hao ambao pia ni watetezi wa haki za binadamu, walikamatwa hata kabla ya kuanza kuandika habari hiyo na walishikiliwa kwa siku kadhaa bila kufunguliwa mashtaka, “kisha wakashtakiwa kwa kushirikiana kutishia usalama wa ndani wa taifa kisa tu kwa ujumbe binafsi uliotumwa na mmoja wao kwa mfanyakazi mwenzake.”

Kesi dhidi yao iliendeshwa kwa saa mbili

Yaelezwa kuwa kesi yao ilifanyika kwa saa mbili na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana shtaka dhidi yao lilibadilishwa na kuwa jaribio la kushindwa kuhatarisha usalama wa taifa bila washtakiwa kujulishwa.

Zaidi ya yote, taarifa hiyo ya ofisi ya haki za binadamu inasema kuwa, waandishi hao wa habari hawakupatiwa fursa ya kujitetea dhidi ya shtaka hilo jipya.

Yaelezwa kuwa kesi yao ilifanyika kwa saa mbili na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana shtaka dhidi yao lilibadilishwa na kuwa jaribio la kushindwa kuhatarisha usalama wa taifa bila washtakiwa kujulishwa.- Wataalamu

Kwa kutambua kuwa kesi hiyo imefanyika kwenye mazingira ambako uhuru wa kupata habari unazidi kubinywa na kutishiwa hasa wakati wa kuelekea uchaguzi wa Rais, wabunge na manispaa, kati ya mwezi Mei na Agosti mwaka huu, wataalamu hao maalum wa Umoja wa Mataifa wametaka haki za waandishi wa habari na vyombo vya habari ziheshimiwe.

Kwa mujibu wa sheria mpya ya vyombo vya habari iliyopitishwa tarehe 14 mwezi Septemba mwaka 2018, waandishi wa habari wanapaswa kuandika habari ambayo ina mizania la sivyo watakumbwa na vikwazo.

Baraza la Taifa la Mawasiliano nalo limepitisha kanuni ya maadili mema kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari wakati wa kipindi cha uchaguzi wa mwaka huu ambayo inazuia wana habari kuchapisha baadhi ya taarifa kwa maslahi ya umma.

Taarifa hizo ni pamoja na kura za maoni au taarifa zozote kuhusu uwezekano wa kupingwa kwa matokeo ya uchaguzi.