Viongozi Sudan Kusini wanyima wananchi chakula kwa makusudi- Ripoti

20 Februari 2020

Mamilioni ya raia wa Sudan Kusini wamekuwa wakinyimwa kwa makusudi huduma za msingi na hata kuachwa na njaa ilihali viongozi wa kisiasa nchini humo wanajinufaisha na mapato ya taifa, imesema kamisheni ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Kusini hii leo.

Ripoti ya nne ya kamisheni hiyo iliyotolewa hii leo huko Geneva, Uswisi na Johannesburg, Afrika Kusini, imesema kuwa ufisadi na ushindani wa kisiasa umechochea ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba ndio vichocheo vikubwa vya mzozo wa kikabila nchini humo.

Mathalani ripoti inasema mamilioni ya dola yameporwa kutoka mamlaka ya mapato ya taifa na kusarambarisha rasilimali ambazo zingaliweza kutumia kulinda na kusongesha  haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni za wananchi wa Sudan Kusini.

Halikadhalika kiwango cha juu cha umaskini na ukosefu wa huduma za msingi kama vile afya na elimu kinazidi kuchochewa na vitendo vya uhalifu wa kiuchumi vinavyofanywa na viongozi wa serikali.

Kamishna Andrew Clapham amesema suala la watu kuachwa na njaa kwa makusudi kulingana na misimamo yao ya kisiasa na makabila yao ni Dhahiri ikiwa ni lengo la kuengua jamii pinzani na pia wale wanaopingana na hali ya kawaida wasiyoitaka.

Ikifafanua kwa kina ripoti hiyo inasema kitendo cha maafisa wa serikali kutumia vibaya fedha za umma kina madhara makubwa katika hali ya kibinadamu Sudan Kusini kwa sababu inaacha watu wa kawaida bila uhakika wa chakula.

Zaidi ya asilimia 55 ya wananchi wa Sudan Kusini, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto hawana kabisa chakula kutokana na sera za makusudi za kuzuia misaada ya kibinadamu kufikia raia wenye misimamo tofauti ya kisiasa au makabila tofauti.

Bwana Clapham amesema kunyima watu chakula kwa makusudi kunaweza kuwa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya binadamu.

Naye Kamishna Barney Afako ameesma kuwa “Sudan Kusini iko katika wakati muhimu ambao viongozi wake wanahitaji kufanya uamuzi mgumu ili kusongesha mbele mchakato wa kisiasa uliokwama wa mkataba mpya wa amani wa kutatua mzozo Sudan Kusini,” huku akisihi pande zote ziongeze juhudi maradufu kupatia suluhu masuala yaliyosalia.

Huku wakikaribisha uamuzi wa hivi karibuni wa Rais Salva Kiir wa kupunguza idadi ya majimbo kutoka pendekezo lake la awali la majimbo 32 hadi 10, kamisheni hiyo imesema pendekezo la kuunda maeneo matatu ya utawala bado ni tata.

Changamoto nyingine wamesema ni suala la mifumo ya usalama iliyopendekezwa, ikiwemo kuundwa kwa majeshi yaliyounganishwa na ulinzi wa viongozi waandamizi wa upinzani.

Kando mwa kusuasua kwa mchakato wa amani, Kamisheni ilipokea pia ripoti ya k wamba baadhi ya wanajeshi wa serikali walipatia wanamgambo wa baadhi ya maeneo silaha nyepesi na nzito ikiwemo AK-47 na maguruneti ili waweze kufanya mashambulizi dhidi ya jamii za jirani hasa wakati wa hama hama ya mifugo.

Halikadhalika vikosi vya serikali na vile vya upinzani vimeendelea kutumikisha jeshini wanaume na wavulana ikiwa ni ukiukwaji wa sheria za haki za binadamu ambapo “kamisheni imenakili matukio ya vikundi vinane tofauti vya jeshi na vikundi vilivyojihami kutumikisha na kupatia mafunzo ya kijeshi watoto wenye umri mdogo wa miaka 12, kitendo ambacho ni kinyume can sheria ya Sudan Kusini na itifaki ya mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto.”

Kuhusu nini kifanyike, Yasmin Sooka ambaye ni mjumbe wa Kamisheni hiyo amesema ukiukwaji wa sheria na ukosefu wa uwajibishaji wahusika ikiwemo pia kutowajibishwa kutokana na vitendo vyao vya zamani ni kichocheo kikubwa cha mzozo Sudan Kusini.

Amenukuu wananchi wa Sudan Kusini ambao amesema, “mara kwa mara wametueleza kuwa uwajibishaji wa wale wanaotekeleza vitendo hivyo ni muhimu ili waaweze kuelewa kwa dhati kuwa kile wanachofanya si sahihi. Kila mtu anaelewa kuwa kuendelea kwa ukwepaji wa sheria kutaendeleza mzozo.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter