Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tabianchi, matangazo ya biashara vyatishia afya ya watoto duniani- Ripoti

Watoto wakicheza kwenye uwanja nchini Namibia.
WHO/Willem Vrey
Watoto wakicheza kwenye uwanja nchini Namibia.

Tabianchi, matangazo ya biashara vyatishia afya ya watoto duniani- Ripoti

Tabianchi na mazingira

Kadri vitisho vitokanavyo na  mabadiliko ya tabianchi na biashara vinavyozidi kushika kasi, nchi nazo zinashindwa kuchukua hatua kuweka mazingira bora kwa afya ya mtoto, imesema ripoti mpya iliyochapishwa kwa ushirikiano kati mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la afya, WHO na jarida la Lancet.

Ikipatiwa jina Mustakabali wa watoto? ripoti imebaini kuwa afya na mustakabali wa kila mtoto na barubaru duniani hivi sasa unakabiliwa na tishio la uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi  mbinu mbovu na za ushawishi za masoko ambazo zinachechemua zaidi kwa watoto ulaji wa vyakula vilivyosindikwa, vinywaji vyenye sukari, vilevi na tumbaku.

“Hakuna hata nchi moja iliyo na mikakati toshelezi ya kulinda afya ya watoto, mazingira yao na mustakabali wao imesema,”  imesema ripoti hiyo iliyoandaliwa na wataalamu zaidi ya 40 wa masuala ya afya ya watoto na barubaru kutoka maeneo mbalimbali duniani na kutolewa New York, Marekani, London,  Uingereza na Geneva, Uswisi.

Mwenyekiti mwenza wa kamisheni hiyo, Helen Clark amesema licha ya mafanikio katika afya ya mtoto na barubaru katika miaka 20 iliyopita, maendeleo yamekwama na kuna mwelekeo wa kurudi nyuma.

Amesema kuwa inakadiriwa ya kwamba, “watoto milioni 250 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao wanaishi katika nchi za vipato vya chini na kati wako hatarini kutofikia ustawi wao kutokana na kudumaa na umaskini. Lakini hofu kubwa zaidi ni kwamba kila mtoto duniani hivi sasa anakabiliwa na vitisho vya sasa vya mabadiliko ya tabianchi na  mashinikizo ya biashara.”

Kwa mantiki hiyo amesema nchi lazima zibadili kabisa mifumo yao kwa afya za watoto na barubaru ili kuhakikisha kuwa si kwamba dunia inalea watoto wao hivi sasa  bali pia inatunza dunia ambayo watairithi siku za usoni.

UN News Kiswahili
Mabadiliko ya tabianchi ni kweli

Shinikizo kwa tabianchi ni tishio la mustakabali wa kila mtoto

 Ripoti hiyo imetumia vipimo vipya kutoka nchi 180 duniani ambapo mataifa hayo yanalinganishwa utendaji wao katika ustawi wa mtoto ikiwemo afya, elimu  na lishe, maendeleo yao kwa kumulika utoaji wa gesi chafuzi, uwiano na pengo la kipato.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakati nchi maskini zinapaswa kuchukua hatua zaidi kusaidi watoto wao kuishi maisha yenye afya, kiwango cha juu cha hewa ya ukaa kutoka mataifa tajiri kinatishia mustakabali wa watoto wote.

Iwapo kwa mujibu wa makadirio ya sasa kiwango cha joto kitazidi nyuzi joto 4 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo mwaka 2100, hii itasababisha madhara mabaya zaidi ya afya kwa watoto, kutokanana kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, mawimbi joto, magonjwa kama vile malaria, denge na utapiamlo,”  imesema ripoti hiyo.

Kipimo hicho kimeonesha kuwa watoto wa Norway, Korea Kusini na Uholanzi wana nafasi bora zaidi ya kuishi na kustawi ilihali watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Chad, Somalia, Niger na Mali wanakabilwa na machungu kupindukia katika makuzi yao.

Akiangazia suala la matangazo ya biashara, Profesa Anthony Costello, ambaye ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo amesema hoja ya viwanda kujidhibiti vyenyewe imeshindwa kwa sababu tafiti zinaonesha kuwa viwanda vimeshindwa kuzuia matangazo yasiyofaa kwa watoto.

“Mfano, licha ya viwanda nchini Australia kutia saini kanuni za kujidhibiti, watoto na barubaru bado wanaona matangazo milioni 51 ya pombe kwa kipindi cha mwaka mmoja tu wakati wa matangazo ya mpira wa miguu, kriketi na raga na hali inaweza kuwa mbaya zaid,” amesema Profesa Costello.

Je nini kifanyike kulinda watoto?

 Kamisheni hiyo imekuja na mapendekezo matano ambayo ni mosi, kuacha utoaji wa hewa chafuzi, pili watoto na barubaru kuwa kitovu cha kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, tatu, sera mpya na uwekezaji katika sekta zote ili kulinda afya na haki za mtoto, nne, kujumuisha sauti za watoto kwenye maamuzi ya kisera na tano kusimamia kwa kina kanuni dhidi ya matangazo ya kibiashara kupitia itifaki mpya ya ziada ya mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto.

 

TAGS: WHO, UNICEF, Lancet, Tabianchi