Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgao wa chakula wasababisha vifo Niger, UNHCR yatoa tamko

Shirika la chakula duniani, WFP likisambaza mgao wa chakula katika jimbo la Ituri, DRC. (21 Machi 2018.)
WFP/Jacques David
Shirika la chakula duniani, WFP likisambaza mgao wa chakula katika jimbo la Ituri, DRC. (21 Machi 2018.)

Mgao wa chakula wasababisha vifo Niger, UNHCR yatoa tamko

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeelezea masikitiko  yake kufuatia taarifa za vifo vya watu wapatao 20 vilivyotokea wakati wa kugombania chakula huko eneo la Diffa nchini Niger.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi imesema miongoni mwa waliofariki dunia ni wanawake na watoto wachanga wakiwemo wakimbizi wanne.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mgao huo wa chakula ulikuwa unatolewa na mamlaka za Nigeria zilizokuwa zinatembelea eneo hilo kugawa msaada kwa wakimbizi kutoka Nigeria.

Huku kukiwa na hofi kuwepo kwa idadi kubwa ya majeruhi, bado ku kuna hofu pia idadi ya wahanga pia inaweza kuongezeka kwa kuwa bado wanapokea taarifa kutoka hospitali na vituo vya afya mjini Diffa.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Niger, Alessandra Morelli amesema pamoja na kushukuru juhudi za wananchi za kujaribu kusaidia wakimbizi, “lakini ombi letu la dhati ni kwamba juhudi hizo lazima ziratibiwe na mamlaka za eneo husika  nchini Niger pamoja na wahudumu wa kibinadamu.”

UNHCR, ambayo haikuhusika katika tukio hilo la mgao wa chakula cha msaada siku  ya jumapili, imekuwa ikitoa huduma za ulinzi na misaada mingine kwa wakimbizi na wakimbizi wa ndani kwenye hilo la kusini-mashariki mwa Niger na tayari lina mfumo ambao unahakikisha kuwa mgao wowote unafanyika bila rabsha.

Eneo hilo la Daffa linalopakana na jimbo la Nigeria la Borno, hivi sasa linahifadhi watu 263,000 ambao wamekuwa wakimbizi kwenye bonde la Ziwa Chad.

Idadi kubwa ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto kutoka Nigeria na wachache hivi karibuni wamekuwa wakiwasili kutoka Chad.

Kwa sasa UNHCR inawapatia msaada wa dharura manusura wa tukio hilo.

Nchini Niger na katika bonde la Ziwa Chad, UNHCR inaongoza harakati za kimataifa za kulinda wale waliokimbia  makazi yao kwa sababu ya mizozo na hofu ya mateso kwenye nchi zao.