Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapiganao kwa misingi ya dini kwingineko wafike Kartapur wajionee dini inavyojenga amani- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiosha miguu na mikono kama taratibua ya kumwezesha kuingia kwenye madhabahu ya hekalu la kalasinga huko Kartarpur  Sahib, jimboni Punjab nchini Pakistani
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiosha miguu na mikono kama taratibua ya kumwezesha kuingia kwenye madhabahu ya hekalu la kalasinga huko Kartarpur Sahib, jimboni Punjab nchini Pakistani

Wapiganao kwa misingi ya dini kwingineko wafike Kartapur wajionee dini inavyojenga amani- Guterres

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametamatisha ziara yake ya siku tatu nchini Pakistani hii leo kwa kutembelea ushoroba wa Kartarpur unaotoa fursa kwa waumini wa madhehebu ya kalasinga kusafiri hadi maeneo takatifu yaliyo kwenye pande zote za mpaka wa Pakistani na India.

 

Akiwa kwenye maeneo hayo ametembelea hekalu la kalasinga au Gurdawa lililopo mji wa Kartarpur nchini Pakistani na kusema kuwa, “ ni heshima kubwa kutembelea eneo hili kati ya nchi mbili hizi ambalo ni ushoroba wa matumaini.”

Amewambia waandishi wa habari baada ya ziara hiyo kuwa, “pindi tunapoona maeneo mengi duniani wakipigana kwa msingi wa dini, ni muhimu kusema kuwa dini inatuunganisha kwa amani na ishara kuu ni hekalu hili.”

Guterres atoa matone ya chanjo dhidi ya polio

Mapema Katibu Mkuu  Guterres ameshiriki katika kampeni  ya utoaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwenye mji wa Lahore.

Kampeni hiyo ya kwanza ya kitaifa ya mwaka inayofanyika mwezi huu wa Februari inalenga kufikia zaidi ya watoto milioni 39 nchini humo katika taifa hilo ambamo mwaka jana pekee kulikuwepo na ongezeko kubwa la visa vya polio na polio pori mwaka jana na mwaka huu pekee tayari kuna wagonjwa 17.

Katika tukio hilo Bwana Guterres alipatia matone ya chanjo wanafunzi watatu, na kisha kupongeza Pakistani kwa harakati zake za kutokomeza ugonjwa huo akiongeza kuwa polio ni ugonjwa ambao jamii ya kimataifa inaweza kutokomeza katika miaka michache ijayo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akimpatia matone ya chanjo dhidi ya polio mmoja wa watoto kwenye shule ya chekechea aliyotembelea leo huko Lahore nchini Pakistani.
UN News/May Yaacoub
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akimpatia matone ya chanjo dhidi ya polio mmoja wa watoto kwenye shule ya chekechea aliyotembelea leo huko Lahore nchini Pakistani.

Amesema azma hiyo ni kipaumbele cha Umoja wa Mataifa na amefurahi sana kuona kuwa ni kipaumbele dhahiri pia cha serikali ya Pakistani.

Hata hivyo ametoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wa kidini na kijamii kuunga mkono kwa dhati serikali  ya Pakistani na serikali nyingine zote duniani kuhakikisha kuwa dunia inaweza kutokomeza ugonjwa wa polio.

Wakati wa ziara hiyo Katibu Mkuu amekutana na wahudumu wa afya walio mstari wa mbele wakitoa chanjo dhidi ya polio na kuelezea mshikamano wake na wahudumu hao ambao sasa idadi yao ni 265,000.

Wahudumu hao wanatembea kaya kwa kaya kuhakikisha kuwa watoto wengi zaidi wanapatiwa chanjo dhidi ya polio na ambapo asilimia 62 ya wafanyakazi hao ni wanawake.

Serikali ya Pakistani  yashukuru Umoja wa Mataifa

Tukio la utoaji wa chanjo lilishuhudiwa pia na Waziri wa Afya wa jimbo la Punjab, Dkt. Yasmin Rashid, ambaye pamoja na kumkaribisha Katibu Mkuu kwenye shule hiyo ya chekechea, ameshukuru Umoja wa Mataifa za kusaidia taifa hilo kufanikisha kampeni yake ya kutokomeza polio.

“Serikali ya Pakistani inashukuru Umoja wa Mataifa kwa msaada wake katika azma ya Pakistani kutokomeza polio. Tumeazimia kufanya kazi kama timu moja chini yap aa moja na tunaamini pamoja tunaweza kuifanya Pakistani itokomeze kabisa polio,”  amesema Dkt. Rashid.

Kwa upande wake, mwakilishi wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO nchini Pakistani, Dkt. Palitha Malipala amesema ziara ya Katibu Mkuu imefanyika wakati amapo mpango wa kutokomeza polio nchini humo unaweka mikakati mipya kwenye operesheni zake na mifumo yake ya kuokomeza polio katika ngazi zote za kisiasa.

 “Kutokomeza polio kumesalia kuwa kipaumbele cha juu cha WHO na ubia wa kimataifa wa kutokomeza gonjwa hilo. Tutaendelea kusaidia serikali ya Pakistani ambayo imeimarisha kampeni hii nchini kote, katika kukabiliana na changamoto za mwaka jana na kuweka mikakati bora ya kuhakikisha kuwepo kwa dunia isiyo na polio kwa kizazi kijacho,”  amesema Dkt. Malipala.

Ikiwa inaendana na mipango ya Umoja wa Mataifa, mpango wa Pakistani wa kutokomeza polio umeazimia pia kuhakikisha watoa huduma wako salama na katu hawawi walengwa wanapofanya kazi yao ya kutoa chanjo.

Eneo hilo la mashariki mwa bahari ya Mediteranea ni eneo pekee duniani ambapo bado lina maambukizi ya ugonjwa wa polio pori, ambapo wagonjwa wamebainika Afghanistani na Pakistani.