Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu bora ni nyenzo muhimu ya kujenga usawa duniani

Mtoto wa umri wa miaka 6 akiwa ameshika kabrasha lake la elimu alilolipokea kutoka UNICEF ikiwa ni sehemu ya msaada wa watoto na familia zilizoathiriwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji.
UNICEF/James Oatway
Mtoto wa umri wa miaka 6 akiwa ameshika kabrasha lake la elimu alilolipokea kutoka UNICEF ikiwa ni sehemu ya msaada wa watoto na familia zilizoathiriwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji.

Elimu bora ni nyenzo muhimu ya kujenga usawa duniani

Utamaduni na Elimu

Hii leo kwenye makao makuu ya  Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kumeanza mkutano wa mwaka wa Umoja wa Mabunge duniani, IPU ambapo suala kuu linalomulikwa ni elimu.

Akifungua mkutano huo wa siku mbili, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Profesa Tijjani Muhammad-Bande amesema elimu ni nyezo muhimu ya kuleta usawa wa ukweli duniani na kwamba ni jukumu la mabunge kuhakikisha rasilimali za kutosha zinaelekezwa kwenye sekta hiyo.

Amesema rasilimali zinahitajika si tu kwa elimu kijumla jumla bali kwa elimu ya mtoto wa kike, elimu, ufundi na ufundi stadi akisema kuwa fedha hizo zinapaswa kujumuishwa kwenye mchakato mzima wa bajeti ya taifa.

Akigusia kuwa elimu ni kipaumbele kikuu cha mkutano wa 74 wa Baraza Kuu anaoungoza, amefurahishwa kwa IPU nayo kuangazia umuhimu wa elimu, ambalo ni lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Hata hivyo amesisitiza kuwa ili vijana wawe na mwanzo mzuri au ustawi mzuri maishani, ni lazima lengo hilo namba 4 litekelezwe vyema kwa kutengeza fedha zinazotosha.

“Nchi moja kati ya nne hazitengi asilimia 4 inayotakiwa ya pato lao la ndani kwa ajili ya elimu na hata ile asilimia 15 ya matumizi ya umma hayaelekezwi kwenye elimu,”  amesema Profesa Muhammad-Bande.

Amekumbusha kuwa iwapo jamii ya kimataifa inataka kushughulikia janga la elimu na wanafunzi waweze kufikia kiwango cha kusoma na kuandika sambamba na ufahamu wa hisabatu duniani, ni lazima kuwekeza kwa watu hususan vijana.

Fursa bora ya elimu

Pamoja na kusisitiza elimu, Rais huyo wa Baraza Kuu amekumbusha kuwa elimu hiyo ni lazima iwe bora na si bora elimu na kwa mantiki hiyo wanafunzi ili waweze kusoma wanahitaji eneo lililo salama, lisilo na ukatili, lenye huduma bora za kujisafi, maji safi na salama pamoja na mtandao wa intaneti.

Ni kwa mantiki hiyo basi ni dhahiri kwamba tunaweza kunufaika na lengo namba 4 iwapo tutalishughulikia kupitia mipango mtambuka kwa kujumuisha sekta mbalimbali za serikali,”  amesema Profesa Muhammad-Bande.

Ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na walimu wenye ueledi na waliopatiwa mafunzo bora sambamba na mitaala ambayo inakidhi mahitaji ya wanafunzi na zaidi ya yote mahitaji ya jamii.

Watoto walio kwenye mizozo

Amegusia pia watoto wasio shuleni akisema kuwa  hakuna jambo lolote linalohalalisha watoto milioni 265 wasiwepo shuleni hivi sasa.

“Iwapo tutashindwa kuwekeza kwa watu wetu, hususan vijana, tutashindwa kutekeleza jukumu la msingi la Umoja wa Mataifa, ambalo ni kusongesha amani na usalama kwa wote,”  amesema Rais huyo wa Baraza Kuu.

Janga la elimu duniani

Katika mkutano huo pia, Rais wa IPU Gabriela Cuevas Barron, amehutubia akimulika kile alichokiita janga la kujifunza au kusoma duniani.

Ametumia takwimu akisema kuwa watu wazima milioni 670 wajinga wasiojua kusoma na kuandika, watoto milioni 258 watakuwa hawako shuleni ifikapo mwaka 2030 huku walimu milioni 69 wakihitajika duniani kote na pengo la bajeti ya kuwezesha kujenga shule na kuboresha maeneo ya shule duniani kote likiwa ni dola bilioni 39.

Amekumbusha kuwa ukosefu wa elimu ndio chanzo cha ukosefu wa usawa na hivyo ni lazima kuhakikisha elimu ni jumuishi na inafikia kila mtu.