Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya majimbo Sudan Kusini bado shubiri katika uundaji wa serikali ya mpito

Makubaliano ya kihistoria ya kuhuisha amani Sudani Kusini yatiwa saini kati ya rais Salva Kiir (kulia) na kiongozi wa upinzani Riek Machar, pichani ewakishikana mikono mjini Addis Ababa 12/9/2018
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Makubaliano ya kihistoria ya kuhuisha amani Sudani Kusini yatiwa saini kati ya rais Salva Kiir (kulia) na kiongozi wa upinzani Riek Machar, pichani ewakishikana mikono mjini Addis Ababa 12/9/2018

Idadi ya majimbo Sudan Kusini bado shubiri katika uundaji wa serikali ya mpito

Amani na Usalama

Ikiwa zimebakia siku 5 kufikia ukomo wa kuwa imeundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Sudan Kusini, suala la idadi  ya majimbo ambalo limekuwa likizusha vuta ni kuvute kati ya serikali na upinzani limechukua sura mpya baada ya Rais Salva Kiir kubadili msimamo wake.

Nchini Sudan Kusini kwenye makazi ya rais yaliyopo mji mkuu Juba, Rais Salva Kiir amejitokeza mbele ya mawaziri na maafisa wa usalama kutangaza msimamo wake kuhusu idadi ya majimbo.

Tangazo lake la mapendekezo ya nchi hiyo kurejea katika majimbo 10 badala ya majimbo 32 ya sasa kama alivyokuwa akitaka awali linalenga kumaliza mkwamo na upinzani, ikiwa zimesalia siku tano kufikia ukomo uliowekwa baada ya kutiwa saini kwa makubaliano mapya ya amani mwezi Septemba mwaka 2018 nchini Ethiopia.

(Sauti ya Salva Kiir)

 “Kulegeza kwetu msimamo hii leo ni moja ya maamuzi machungu niliyowahi kufanya lakini ni muhimu iwapo hiki ndicho kitarejesha amani na umoja wa watu wetu. Nimepigana maisha yangu yote kukomboa nchi hii na nitaendelea kusimama dhidi ya nguvu zozote zenye lengo la kuharibu uhuru wetu tulioupata kwa kuvuja jasho. Sitakubali kushuhudia uharibifu wa taifa hili ambalo nimejitolea mhanga kulikomboa.”

Hoja ya idadi ya majimbo imekuwa mwiba tangu kutiwa saini kwa makubaliano mapya ya amani mwaka juzi na imethibitisha kukwamisha uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Upande wa upinzani  unashikilia msimamo wa majimbo 10 au 23.

Rais Kiir anashutumu upinzani kwa kuweka taifa hilo rehani kutokana na msimamo wao.

(Sauti ya Salva Kiir)

 “Msisitizo wao wa kutaka kurejea katika majimbo  10 ni mkakati wa watu ambao hawatutakii mema zaidi ya kutaka machungu na uharibifu.Uamuzi wangu wa leo  utazuia nia mbaya kama hizo na kutufanya tuwe na  mnepo dhidi ya vitisho vyao.”

Hata hivyo Rais Kiir amesema uamuzi wa kurejea katika majimbo  10 unaweza kuwa ni wa muda tu na kwamba unalenga kufanikisha uundwaji wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ambayo ndiyo itaamua idadi ya majimbo.

Ametoa wito kwa pande nyingine nazo kuthibitisha utayari wao wa kulegeza msimamo.

Upande wa upinzani bado haujatoa taarifa yoyote kufuatia tangazo la Rais Kiir lakini utakuwa kwenye shinikizo la kuamua iwapo wanataka kujiunga na serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa wiki hii.