Virusi vya COVID-19 sio hatari kama vilivyo virusi vingine vya aina hiyo-WHO

17 Februari 2020

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema inaonekana kwamba virusi vya corona COVID-19 sio hatari kama vilivyo virusi vingine vya aina hiyo ikiwemo vile vinavyosababisha homa ya mafua, SARS au virusi vya corona vinavyosababisha matatizo ya kupumua MERS na kuongeza kwamba asilimia 80 ya wagonjwa wana viwango vya chini vya  virusi na watapona.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema takwimu mpya kutoka China zinaangazia baadhi ya pengo katika uelewa lakini bado zingine zinasalia akiongeza kwamba wataalamu wa WHO wanashirikiana na wataamu wa China kuelewa bora pengo hizo na kuimarisha uelewa wa mlipuko.

China imeripoti visa 70, 635 na vifo 1772 ambapo katika kipindi cha saa 24, China imeripoti visa vipya 2051 ikiwemo vile ambavyo vimethibitishwa na kituo cha afya na maabara. 

Asilimia 94 ya visa vipya vimetokea jimbo la Hubei na kwamba nje ya China, wamepokea ripoti ya visa 694 kutoka nchi 25 na vifo vitatu.

WHO imesema wakati ikiendelea kupokea taarifa zaidi kutoka China, wanapata picha kamili ya mlipuko na mwenendo wake na inakoelekea. DKt. Tedros amesema kwamba China imechapisha taarifa ya takwimu kwa undani juu ya visa 44,000 vilivyothibitishwa vya COVID-19 akiongeza kwamba, “takwimu hizo zinatupatia picha halisi ya umri wa watu walioathirika, usugu wa ugonjwa na idadi ya vifo. Kwa maana hiyo ni muhimu sana katika kuwezesha WHO kutoa ushauri nasaha kwa nchi. Tunahimiza nchi zote kutoa takwimu zao kwa umma."

Kwa mujibu wa takwimu kuna kupungua kwa visa vipya, hata hivyo WHO imeonya kuangalia hili kwa karibu kwani bado ni mapema.

WHO inaendelea kusadia nchi kujiandaa kwa kutuma vifaa vya uchunguzi kwenye maabara kote ulimwenguni. Pia wanatoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na kutuma vifaa kinga na kufanya kazi na wazalishaji kuhakikisha uwepo wa bidhaa.

Dkti. Tedros amekumbusha kwamba kuna fursa na kwamba raslimali zinahitajika sasa kuhakikisha kwamba nchi zinajiandaa. Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kufadhili ombi la dola milioni 675 kwa ajili ya kusaidia nchi kujiandaa na kwamba, “hatujashuhusia uhitaji wa ufadhili tunaohitaji. Kama ninavyokumbusha tuna fursa sasa. Tunahitaji raslimali sasa kuhakikisha nchi zinajiandaa sasa. Hatujui fursa huu itakuwepo mpaka lini. Hebu tusiipoteze.”

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF  limesema linahitaji dola milioni 42.3 kwa ajili ya kuimarisha msaada kukabiliana na mlipuko wa COVID-19 ambapo Mkurugenzi Mkuu, Henrietta Fore amesema, “lengo la sasa ni kupunguza maambukizi kutoka binadamu mmoja hadi mwingine lakini pia kuwaweka watoto katika maeneo ambamo ufikiaji wao wa huduma za msingi hauvurugiki.”

Ili kukabiliana na athari za mlipuko, UNICEF inatarajia kusaidia katika fursa za elimu ya mbali kwa watoto ambao hawawezi kufika shule na kutoa msaada wa afya ya akili na ya kisaikolojia kwa watoto na familia zilizoathirika.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter