Kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa Afghanistani ndio suluhu ya pekee- Guteres

17 Februari 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uwezo wa jamii ya kimataifa kusaidia kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa Afghanistan utakuwa ni jaribio kubwa la mkataba wa kimataifa wa wakimbizi.

Bwana Guterres amesema hayo leo huko Islamabad nchini Pakistani wakati wa mkutano wa kimataifa wa kuadhimisha miaka 40 ya taifa hilo la Asia kuhifadhi wakimbizi kutoka Afghanistani.

 “Wananchi wa Afghanistan hawawezi kutelekezwa. Sasa ni wakati wa jamii ya kimataifa kuchukua hatua na kutekeleza,” amesema Bwana Guterres akidokeza kuwa kiwango cha wakimbizi wa Afghanistan kurejea nyumbani kimekuwa cha chini zaidi hivi sasa na kuvunja rekodi ya kihistoria.

 Kwa mantiki hiyo amesema kuwarejesha nyumbani kwa hiari ni ahadi ya wajibu mkubwa kwa mataifa ambayo hivi sasa yamebeba mzigo wa kuwahifadhi.

“Juhudi zetu za kuwarejesha na kuwajumuisha kwenye jamii, zikiongozwa na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR zinalandana na muundo wa amani na maendeleo wa taifa la Afghanistani,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa hivi sasa wanashirikiana na jukwaa mahususi la usaidizi la kikanda ili kusaidia kurejea nyumbani kwa hiari kwa wakimbizi wa Afghanistani na kuhakikisha wanajumuishwa vyema kwenye jamii huku wakiendelea kupatia usaidizi wakimbizi wengine na jamii zinazowahifadhi huko Iran na Pakistani.

Amekumbusha kuwa harakati za amani zinazoweza kufanikisha mashauriano baina ya waafghanistani wenyewe zitafungua njia lakini amani na utulivu endelevu vinategemea ujumuishaji bora wa kazi za kibinadamu, maendeleo na amani.

Katibu Mkuu  huyo wa Umoja wa Mataifa amesema iwapo hilo litafanyika vyema, basi utakuwa ni muundo bora zaidi wa mfano kwa maeneo mengine duniani.

“Lazima tuwe wahalisia, tunafahamu kuna changamoto kubwa mbele lakini ujumbe kutoka mkutano huu na uwepo wa maafisa wengi waandamaizi wa serikali kutoka maeneo mbali mbali duniani ni ushahidi tosha wa agano la matumaini na azma ya ubia mpya wa mshikamano na mustakabali bora kwa watu wa Afghanistani na Pakistani na dunia  nzima,” ametamatisha Bwana Guterres.

Raia milioni 2.7 wa Afghanistan wamesajiliwa kuwa ni wakimbizi walioko maeneo mbalimbali duniani ambapo milioni 1.4 kati yao hao wanaishi nchini Pakistani.

Akizungumzia hali hiyo, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR, Filippo Grandi amesema kuwa mahitaji yao hao na yale  ya jamii zinazowahifadhi ndio msingi wa mkutano huo unaofanyika Islamabad.

“Kusaka suluhu ni muhimu sambamba na kuchagiza mchakato wa amani nchini Afghanistani ili uendelee,” amesema Bwana Grandi akiongeza kuwa ukimbizi nchini humo unaweza kupatiwa suluhu kwa kupatikana amani na amani inaweza kuimarishwa kwa kutatua suala la ukimbizi.

Kwa miaka 40 sasa wananchi wa Afghanistani wamekuwa wakisaka hifadhi Pakistani kutokana na mzozo nchini mwao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter