Ukarimu wa Pakistan kwa wakimbizi haukujali gharama wala usalama:Guterres

16 Februari 2020

Kwa miaka 40 Pakistan imekuwa ikihifadhi mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan na ukarimu wao haukujali gharama za mzigo huo za kiuchumi au hatari za kiusalama amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Akizungumza mjini Islamabad katika ziara yake ya kwanza nchini humo kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “upendo wa Pakistan umetokana na ukarimu na mshikamano wake kwa mamilioni ya wakimbizi wakiruhusu kushirikiana rasilimali chache walizo nazo, kubeba athari za kiuchumi kwenye jamii zao lakini pia hatari ya athari za kiusalama kutokana na mgogoro wa Afghanistan.”

Mabadiliko ya tabianchi

Guterres amesema nchi hiyo yenye ukarimu mkubwa haistahili kubeba madhila mengine lakini mabadiliko ya tabianchi hayalitambui hilo amekumbusha athari walizozipata watu wa Pakistan walipokumbwa na farukiko makubwa na kusema anahisi si haki na kwa sasa ameongeza “Pakistan ikomiongoni mwa nchi zilizo katika mstari wa mbele wa kuathirika na mabadiliko ta tabianchi. Sio Pakistan inayosababisha mabadiliko ya tabianchi bila shaka ina mchango kidogo, lakini iko mstari wa mbele katika athari za mabadiliko ya tabianchi”.

Mbali ya mabadiliko ya tabianchi Katibu Mkuu amezungumzia ajenda ya maendeleo endelevu ambayo ukomo wake ni 2030 ambayo ni mchanganyiko wa malengo 17 ya maendeleo yanayojumuisha vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ambaye amesema huenda kwa sasa ni tishio kubwa la Amani na usalama wa kimataifa, utulivu na mafanikio.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

 

Malengo ya maendeleo endelevu

Katibu Mkuu amesema malengo hayo yanagusa kila nyanja ya maendeleo ya binadamu yanalenga umasikini, pengo la usawa, njaa na afya.

Yanashughulikia masuala muhimu kama elimu bora, ajira zenye hadhi, uchumi sawia na usawa wa kijinsia, pia yanakabiliana na mabadiliko ya tabianchi na yanazifanya suluhu za asili kuwa kitovu cha mkakati wetu, yanachagiza haki, taasisi imara na ushirikiano ambao utawezesha nchi zote kupiga hatua endelevu na amehimiza kwamba “Maendeleo endelevu ni muhimu kwa nchi zote na kwa kila jamii, hakuna nchi inayoweza kusema kwamba haina pengo la usawa au masikini mijini walioachwa nyuma au haina matatizo ya uchafuzi wa hali ya hewa au mabadiliko ya tabianchi. Na hakuna nchi inayoweza kusema ina kinga dhidi ya shinikizo za kimataifa ambazo zitaathiri mafanikio yake. Leo hii changamoto za maendeleo endelevu haziheshimu mipaka na hazijikiti kwa nchi moja tu”

Ili kushughulikia changamoto hizi Guterres amesisitiza kwamba jawabu ni ushirikiano ambao unatambua kwamba wote tunaitumia dunia hii moja na tunahitaji kushirikiana kila kona na kila sekta ili kufanikisha ndoto zetu.

Pakistan imekumbatia SDGs

Katibu Mkuu amesema Pakistan imekumbatia malengo ya maendeleo endelevu tangu mwanzo “Mwaka 2016 Pakistan ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kujumuisha SDGs katika ajenda ya maendeleo ya kitaifa na kuyatambua kama ni malengo ya maendeleo ya kitaifa, na mwaka 2018 ilizindua mkakati wa kitaifa wa SDGs kwa kutoa kipaimbele cha malengo hayoa nchi nzima ikiweka kipaumbele katika kutokomeza umasikini ili kutomuacha yeyote nyuma kupitia mkakati wake uitwao Ehsaa ambao umepanua wigo wa hifadhi ya jamii na kuunga mkono maendeleo ya binadamu.”

Mbali ya hapo Pakistan pia imeanzisha mpango wa kitaifa wa maendeleo kwa vijana “Kamyab Jawan” ambao lengo lake ni kuzalisha ajira milioni 10 kwa vijana katika kipindi cha miaka mitano. Na imepiga hatua kubwa katika kupunguza kiwango cha kudumaa na utapiamlo.

Pia inapata mafanikio katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga asante kwa programu yake ya wahudumu wa afya wanawake ambayo imesaidia kuongeza idadi ya wakunga wenye ujuzi kwa kiasi kikubwa.

Katibu Mkuu Antonio Guterres(katikati) akikutana na wakimbizi mjini Islamabad wakati wa ziara yake ya kiofisi nchini Pakistan. Leo hii Pakistan ni nchi ya pili inayohifadhi wakimbizi wengi duniani
Mark Garten).
Katibu Mkuu Antonio Guterres(katikati) akikutana na wakimbizi mjini Islamabad wakati wa ziara yake ya kiofisi nchini Pakistan. Leo hii Pakistan ni nchi ya pili inayohifadhi wakimbizi wengi duniani

Mafanikio kila kona Pakistan

Kastibu Mkuu amesema ametiwa moyo na mafanmikio makubwa nchini Pakistan katika nyanja mbalimbali ikiwemo mkakati wa mwaka huu wa huduma za afya kwa wote, pia umasikini na vifo vya watoto vimepungua sana, watu wengi wanapata fursa za nishati , elimu na ajira zenye hadhi zinaongezeka. Licha ya hatua hizo amesema kasi ya mafanikio hayo bado hairidhi Pakistan na kwingineko duniani.

Amegusia pia Pakistan inakabiliwa na changamoto hasa za HIV na polio, pia mmomonyoko wa mazingira, utoaji elimu, ujuzi na ajira kwa wote katika taifa hilo lililona vijana wengi zaidi duniani.

Katibu Mkuu ameonya kwamba “kimataifa tumetoka nje ya mstari hususan katika maeneo ya njaa, usawa, bayoanuai na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Kutokuwepo usawa wa kijinsia katika biashara, majumbani, mashuleni na aserikalini, katika sekta ya teknolojia wanawanyima wanawake na wasichana haki zao na fursa kote duniani.”

Pia amesema makundi yasiyojiweza kama wahamiaji, vijana na watu wenye ulemavu wanasalia katika hatari ya kuachwa nyuma.

Juhudi zetu za pamoja hazikaribii kiwango tunachohitaji kutimiza SDGs ifikapo 2030” ameonya Guterres akiongeza kwamba kwa mujibu wa baadhi ya makadirio “Kwa kasi ya sasa tutatimiza nusu tu ya malengo hayo, na kwa sababu hiyo mwaka huu tumezindua muongo wa hatua za utimizaji wa SDGs. Ikiwa imesalia miaka 10 tu kufika 2030 kuha haja ya haraka ya kuongeza hatua na kila taifa , kila jamii na kila mtu anaweza na anapaswa kuchangia.”

Afghanistan, Badakhshan mwaka 1990 familia ya wakimbizi ikiondoka nyumbani kuelekea ukimbizini Pakistan ili kuokoa maisha yao
Reza/Webistan
Afghanistan, Badakhshan mwaka 1990 familia ya wakimbizi ikiondoka nyumbani kuelekea ukimbizini Pakistan ili kuokoa maisha yao

Muongo wa hatua

Akiainisha kinachohitajika kufanywa Katibu Mkuu amesema muongozo uko bayana, Mosi kumchagiza kila mtu kuhusu juhudi za pamoja, pili kudai uharaka na hatua na kuwawajibisha viongozi na tatu kuyafanyia kazi mawazo iliyawe suluhu endelevu “tunahitaji kubaini nini kinafanya kazi na kuongeza suluhu na uwekezaji ili kwamba tuweze kuwafikia watu wote duniani. Na katika hili kukusanya rasilimali ili kuziba pengo la dola trilioni 2.5 kwa mwaka ni muhimu sana.”

Kwa upande mwingine amehimiza umuhimu wa kuzisaidia nchi zinazoendelea ili ziweze kukusanya rasilimali za ndani kupitia utawala bora na ukusanyaji kodi.

Wakati huohuo amesema zinahitajika nyezo bunifu za masuala ya fedha ili kusaidia kupunguza hatari za uwekezaji binafsi katika nchi zinazoendelea  ili kuweka uzito wa fedha katika SDGs.

Guterres amesema licha ya changamoto lukuki zinazoikabili dunia hivi sasa ana Imani na kizazi hiki”Ninaimani kubwa kwamba tunaweza kuwa kizazi ambacho kitatokomeza umasikini na njaa na kukabiliana na pengo la haki na usawa, lakini haitakuwa mteremko kibarua kitakuwa kigumu.”

Ametaka kushughulikiwa kwa changamoto zinazoikumba dunia hivi sasa ikiwemo mivutano ya kimataifa, hali yua kutoamianiana kimataifa na hata miongoni mwa watu na viongozi wao.

Pia amesema ni muhimu kushughulikia changamoto ya mapinduzi ya nne ya viwanda na kuhakikisha yanakumbatiwa huku hatari za ukiukwaji wa haki za binadamu na pengo la usawa kote duniani zikipunguzwa. Na mwisho amesema dharura ya mabadiliko ya tabianchi. “Hakuna nchi ambayo ina kinga dhidi ya mabadikliko ya tabianchi na ndio maana kila wakati ninawataka viongozi wa dunia kuchukua hatua kabla hatujachelewa."

Wakati ni sasa la sivyo tumeangamia

Amesema kwa bahati mbaya baada ya mafanikio ya Paris 2015  mkyano wa COP25 Madrid ulikuwa wa kuvunja moyo akisema “dunia yetu inawaka moto lakini wafanya maamuzi wengi wanaendelea kuleta mchezo. Suluhu pekee ni maamuzi ya pamoja ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi hatua za serikali, sekta ya biashara na wawekezaji na mameya na magavana lakini pia wananchi kila mahali”

Amezitaka serikali katika mkutano ujao wa COP26 utakaofanyika Glasgow kuhakilisha lazima zinaleta mabadiliko yanayohitajika duniani na ambayo watu wanayataka. Na amezitaka nchi wachangaji wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi kuongoza juhudi hizo.

Amesisitiza kwamba “tuko katika vita vya maisha yetu, mustakbali wetu uko njiapanda, lakini naamini kwamba ni vita ambavyo tunaweza kuvishinda, teknolojia iko upande wetu. Hivyo wakati tukitafakari mbele 2030 hebu tutafakari kwa matumaini na dhamira tukijua kwamba tumekabili changamoto nyingi hapo kabla na tunaweza kufanya hivyo tena.”

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter