Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maktaba iliyokarabatiwa na walinda amani wa UNMISS ni fursa ya 'kuepuka' hali ukimbizi

Walinda amani wa UNMISS wamekarabati maktaba na kutoa vitabu vipya na vikukuu kwa ajili ya wanafunzi kwenye kituo cha ulinzi wa raia.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Walinda amani wa UNMISS wamekarabati maktaba na kutoa vitabu vipya na vikukuu kwa ajili ya wanafunzi kwenye kituo cha ulinzi wa raia.

Maktaba iliyokarabatiwa na walinda amani wa UNMISS ni fursa ya 'kuepuka' hali ukimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Walinda amani wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS wamekarabati maktaba na kuijaza vitabu vipya na vikukuu ili watoto wanoishi ndani ya vituo vya ulinzi wa raia vya Umoja wa Mataifa Juba waweze kupata fursa bora katika maisha yao. 

Nyakhan Yien Jiek, ni mwalimu wa shule ya msingi ambaye alivutiwa na kitabu kilichoangazia barubaru kutoka Marekani cha “Diary 

of a Wimpy Kid” ambaye uzoefu wake ni kitu kigeni kwa mwanamke huyo anayeishi kwenye kituo cha ulinzi kwa familia zilizofurushwa Juba.

Nyakhan yuko katika hali bora kuliko watu wa umri wake kwani alifanikiwa kupata mafunzo ya kuwa mwalimu na katika umri wa miaka 23 amejitoa kwa ajili ya kukipa kizazi kijacho fursa alizozikosa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini,“Elimu ni muhimu sana kwa sababu kwa kuwapa wengine maarifa inakufanya uwe unashughulika shule na utawaza tu kuhusu shule.”

Mamia ya watoto wanahudhuria shule ya msingi ya Hope katika kituo hicho cha ulinzi wa raia. Wengi wakiwa wamezaliwa hapo baada ya wazazi wao kusaka hifadhi kukimbia machafuko ya mwaka 2013, Na wengi hawajapata kushuhudia maisha nje ya kituo.

Licha ya kwamba wanapata huduma za msingi ikiwemo chakula, maji, huduma ya afya ya msingi na elimu, lakini wameshindwa kufikia uwezo wao kamili maishani.

Kwa kutambua utayari wa watoto kusoma mshauri wa polisi wa Umoja wa Mataifa Elisabeth Joyce Nilssen kutoka Norway aliwaomba wafanyakazi wenzake wa UNMISS kutoa vitabu vyao vikukuu na ikawa mradi mkubwa zaidi ambapo walinda amani wengine walichukua fursa hiyo kubadili maisha ya watoto,“Kuna sehemu ya kunywa chai ambapo kunakuwa na vijana wengi. Siku moja nilikuwa nimeketi ninazungumza nao na walikuwa wamekata tamaa kwa sababu hawakuwa na uwezekano wa kwenda Chuo Kikuu kwa sababu hawana fedha. Lakini nikawauliza na vipi kuhusu kusoma vitabu. Wakasema wangependa kusoma vitabu lakini hawana vitabu vyenyewe. Kisha nikawauliza iwapo nikileta vitabu kama wangependa kuvisoma. Wakasema hiyo ingekubwa nzuri, hapo nikapata wazo labda ninaweza kukarabati maktaba hapa kwa sababu watu wanataka kusoma kingereza lakini hawana fursa hiyo na hapo ndipo wazo hilo lilitokea.”

Luteni Kanali Edward Carpenter ni mmoja wa walinda amani kwenye UNMISS waliosaidia kuchangia vitabu,“Nilitoa kila kitu ambacho nilikuwa nacho, nilipata vitabu vingine kutoka kwa wafanyakazi wenzangu kutoka Australia na wakati wa Krismasi nikaweka ujumbe kwenye mtandao wa twitter na kuwaomba marafiki zangu kutuma vitabu vyao. Walituma vitabu vingi sana na kuna vingine vinakuja na tunajaribu kujaza hii shule ili vijana wa kiume na kike ambao wanataka kujifunza kingereza, wasome kingereza na kukwepa maisha ya kambini kupitia vitabu na wana fursa hiyo.”

Kwa upande wao, walimu katika shule wanasema maktaba itasaidia kuwapa matumaini wanafunzi. James Kot Nyuon, ni mwalimu katika shule ya msingi ya Hope, “Wale ambao wamepata kiwewe watafurahishwa na baadhi ya vitabu wakivisoma. Najua maisha ni magumu sana. Kwa sababu ya elimu hiyo watu wanahisi hawaishi maisha magumu sana. Kwa sababu ya UNMISS watu wanahisi wanafuraha, UNMISS imewasaidia. UNMISS wwapo nasi, wakitulinda kiusalama, wanatupatia huduma kama vile vitabu, kwa hiyo watu wanafurahi wakati wako shule.”