Wazuieni nzige sasa au mbebe gharama kubwa ya kusaidia mamilioni Afrika Mashariki baadaye:WFP/FAO

14 Februari 2020

Itakuwa gharama ndogo kwa sasa kulisaidia shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO   kupambana na nzige Afrika Mashariki  kuliko kuwasaidia mamilioni ya watu katika ukanda huo baada ya mazao yao yote kusambaratishwa, ameonya mkurugenzi mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP David Beasley.

Bwana Beasley amesema FAO inahitaji dola milioni 76 kusaidia kukomesha nzige hao. Kisipofanyika chochote sasa WFP inahitaji mara 15 zaidi ya kiwango hicho ambacho kitakuwa Zaidi ya dola bilioni 1 kuwasaidia watu walioathirika kwa kupoteza mazao yao na uwezo wa Maisha yao. Kuzuia zahma kubwa Afrika ya Mashariki ni uwekezaji bora zaidi ya kukabiliana na athari katika maisha ya mamilioni ya watu wa ukanda huo.”

Hadi sasa FAO imeshakusanya dola milioni 22 katika ya milioni 76 inazozihitaji kwa ajili ya juhudi za kukabiliana na nzige Afrika Mashariki. WFP imeonya kwamba endapo hali hii haitadhibitiwa basi madhara yake yanaweza kuwatumbukiza watu wengine milioni 13 zaidi katika hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

Mtandao wa kikanda wa masuala ya uhakika wa chakula na lishe (FSNWG) leo umeonya kwamba mazalia ya nze sasa yanaongezeka Somalia, Kenya na Ethiopia na mazalia mapya yameashaanza kushuhudiwa Eritrea, Djibouti na Kaskazini Mashariki mwa Uganda.

Bwana Beasley anasema “Tukitazama mbele na kwa mujibu wa utabiri wa mazingira mazuri ya kuzaliana magenge ya nzige yanatarajiwa kuongezeka kwenye maeneo ambayo tayari yameathirika lakini pia kusambaa katika maeneo jirani . Pia kuna hatari kubwa kwamba nzige hao watasambaa Sudan Kusini " Na WFP, FAO, mtandao wa tahadhari ya mapema ya baa la njaa FEWS NET na IGAD wameonya kwamba hiyo itakuwa balaa kubwa kwa taifa ambalo tayari limeathirika vibaya na vita, na majanga mengine hivi karibuni.

Utabiri unaonyesha kwamba nzige wanatarajiwa kuzaliana na kusambaa Zaidi katika miezi ijayo

Nzige wa jangwani wanachukuliwa kuwa ni wadudu hatari Zaidi wanaohamahama duniani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter