Radio ni moja ya chombo cha siku zijazo, hebu tuilinde- UNESCO

13 Februari 2020

Mbinu tofauti za kusambaza taarifa kupitia radio iwe ni katika mita bendi ya AM au FM au kwa kupitia teknolojia za kidijitali au kwenye wavuti zinaendana na utofauti katika yaliyomo kwenye programu ambazo zinazalishwa na wingi wa maoni, utamaduni na yale yanayotangazwa.

Hiyo ni sehemu ya ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu wa Shrika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay katika kuadhimisha siku ya radio duniani hii leo Februari 13.

Bi Azoulay amesema radio ni njia ya aina yake ya kuchagiza tamaduni tofauti na kwamba

(Sauti ya Bi Azoulay)

“Sote tunapenda radio, inaunga mkono ndoto zetu, inaunga mkono taarifa na majadiliano lakini pia ni kifaa muhimu kwa ajili ya utofauti, ni sauti kwa wale wasio na sauti, kwa walio wachache, kwa watu wa jamii za asili ambao pengine wasingeweza kujieleza na hii ndio sababu UNESCO inaunga mkono radio kote ulimwenguni.”

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema radio inazipa jamii uhuru hususan zile za asili kuimarisha utamaduni na mawazo yao kwa kupitia lugha zao. Aidha amesema ni sawa na radio za kijamii ambazo hutangaza maswala ya makundi mengi katika jamii ambayo sauti zao huenda zisisikike iwapo kungekuwa hakuna radio.

UNESCO imesema kwa kuwaalika wasikilizaji kupanua wigo wao na kujifunza mtazamo tofauti na kuchagiza uelewa wa tamaduni tofauti, radio ni chombo na kiutu kinachosaidia katika kukabiliana na unyanyapaa na ubaguzi na kwamba utofauti huo unahitaji kuonekana katika matangazo yake pamoja na miongoni mwa wanaobuni vipindi iwe ni fundi mitambo, wazalishaji wa vipindi, waandishi habari au wanasa sauti, kila mtu ana nafasi muhimu katika kufanikisha hilo.

Bi Azoulay amesema ni muhimu kwa sekta ya radio kuonyesha utaofauti huu kama mfano wa jamii zetu

(Sauti ya Bi Azoulay)

“Bila radio, dunia haingekuwa huru kama ilivyo wala isingekuwa na tamaduni tofauti, radio ni moja ya chombo cha siku zijazo ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba inadumishwa.”

Kwa mantiki hiyo UNESCO imeamua pia kuangazia katika kuimarisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya radio.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter