Leo ni siku ya Radio duniani, bado ni chombo kinachounganisha jamii:UN

13 Februari 2020

Ikiwa leo ni siku ya Radio duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema   Radio inasalia kuwa chombo muhimu katika jamii kinachowaleta watu pamoja.

Katika siku hii ambayo mwaka huu inajikita na umuhimu na mchango wa Radio za kijamii Guterres amesema

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Katika enzi za mageuzi ya haraka ya vyombo vya Habari, Radio inakuwa ni sehemu maalum katika kila jamii kama chanzo cha cha Habari muhimu na taarifa.”

Ameongeza kuwa lakini radio pia ni chanzo cha uvumbuzi ambao uliendeleza mazungumzo na wasikilizaji na taarifa zilizotokana na watumiaji wa chombo hicho kwa miongo kadhaa kabla ya kuwa maarufu. Amesema chombo hicho pia kinaleta utangamano katika jamii

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

Redio inatoa taswira nzuri ya utofauti katika mundo wake, lugha zake, na miongoni mwa wataalam wenyewe wa redio.”

Bwana Guterres amesema hii inatuma ujumbe muhimu kwa dunia kwamba tunapojitahidi kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi radio inajukumu muhimu la kufanya kama chanzo cha habari na mchagizaji.

Amesisitiza kuwa “Katika siku hii ya Radio Duniani hebu tutambue uwezo wa radio katika kuchagiza utofauti na kusaidia kujenga dunia ya amani na jumuishi.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud