Umoja wa Mataifa wahofia kinachoweza kutokea kutokana na ndege zake kuzuiliwa Libya

12 Februari 2020

Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema unasikitika kwamba ndege zake ambazo zinasafirisha maafisa wake kuingia na kutoka Libya, hazijaruhusiwa kutua nchini Libya na jeshi lililojitangaza lenyewe la Libyan National Army, LNA linaloongozwa na kamanda Khalifa Haftar.

“Kitendo hiki kimerudiwa mara kadhaa katika wiki zilizopita.” Imesema taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL iliyotolewa leo mjini Tripoli.

Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi mkubwa kuwa kuzuia ndege zake kuingia na kuondoka Libya kutakwamisha kwa kiasi kikubwa  juhudi zake za kutoa msaada wa kibinadamu katika wakati huu ambapo maafisa wake wote wanafanya kazi kwa bidii kusukuma mbele mazungumzo ya ndani ya Libya na kutoa misaada ya kibinadamu inayohitajika sana kwa raia ambao wameathirika na wako hatarini kutokana na mgogoro.

Hivi karibuni, mzunguko wa kwanza wa mazungumzo kati ya Kamisheni ya pamoja ya kijeshi au 5 + 5, ulihitimishwa ambapo mjini Geneva Uswisi ambapo pande zote mbili zilikubaliana kuendelea na mazungumzo ili kufikia makubaliano kamili ya usitishaji mapigano ambapo na hivyo UNSMIL ikapendekeza mzunguko wa pili wa mazungumzo uwe tarehe 18 mwezi huu wa Februari.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud