Ubora wa miji ni pamoja na urahisi wa usafiri:UN-HABITAT

12 Februari 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT limesema ubora wa miji ni pamoja na kuhakikisha usafiri kwa wakazi wa miji hiyo ni salama na endelevu lakini pia unaozingatia mazingira na kuwapunguzia adha watu wake.

Kauli hiyo imetolewa shirika la makazi la Umoja wa Mataifa huko Abu Dhabi kunakoendelea kongamano la kimataifa la miji. Katika kongamano hilo UN-Habitat kwa kushirikiana na Idara ya Abu Dhabi ya manispaa na usafiri wamezindua rasmi sanamu mpya ikiashiria usafiri wa baiskeli , kazi ya Sanaa ambayo ni ishara ya mradi wa kongamano hilo na miji.

Afisa kutoka manispaa ya mji huo Salem Al Junaib amesema kupitia mradi maalum wa Abu Dhabi wanajenga mamia ya njia za waendesha baiskeli mjini humo na kuongeza kwamba

(SAUTI YA SALEM AL JUNAIB)

Tuna takribani kilometa 400 za njia za baiskeli ambazo tumezitenga hapa Abu Dhabi na njia hizo zitasambazwa mji mzima, zingine katika maeneo yenye foleni kubwa, karibu na barabara kuu, kwa lengo la kuwarahisishia watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine popote watakako.”

Sanamu hiyo ambayo ni kazi ya sanaa ya Ai Weiwei imepewa jina “baiskeli daima” na imetenngenezwa kwa kutumia ringi 720 za baiskeli ambazo ni za chuma na sanamu hiyo ukiingalia inakupa taswira ya baiskeli inayotembea.
UN-HABITAT inasema sanamu hiyo katika kongamano la 10 la miji , WUF10 ni ya kuchagiza watu kutumia usafiri wa baiskeli kwa ajili ya kulinda mazingira , ni salama na kwa afya zao. Christine Knudsen ni afisa wa UN-HABITAT katika kongamano hilo

(SAUTI YA CHRISTINE KNUDSEN)

“UN-Habitat tumejikita katika jukumu letu na msaada wetu kwa lengo la maendeleo namba 11 la miji salama, endelevu na yenye mnepo. Hii ni fursa nzuri ya kuonyesha jinsi gani tunayaangalia maeneo ya umma, usafiri mijini na sanaa za umma kwa ajili ya kuleta jamii pamoja kuweka mazingira salama na bora ambako jamii zinakutana.

Kongamano hilo la 10 la kimataifa la miji linafanyika katika nchi za Kiarabu kwa mara ya kwanza.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud