Jamhuri ya Kongo yaongeza chanjo ya polio katika maeneo ya mpaka wake na Cameroon na CAR

11 Februari 2020

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema hii leo wataalamu wa chanjo wameanza kuzunguka katika vijiji vya Sangha maeneo ya kaskazini mwa Jamhuri ya Congo wakitoa chanjo dhidi ya polio inayoweza kuenezwa kutoka katika nchi za jirani.

Eneo la Sangha linapakana na Cameroon na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako kulionekana kuwa na virusi vya polio mwaka jana 2019.

Mtoa chanjo Yvone Komba na timu yake wametembelea zaidi ya vijiji 16 na kuwachanja zaidi ya watoto thelathini katika siku ya tatu na ya mwisho ya kampeni. Tofauti na miaka iliyopita, Bi Komba amesema jamii sasa zinapokea vizuri chanjo na akatoa shukrani kwa elimu ya afya iliyosambazwa kwa jamii na pia kampeni za mara kwa mara za polio.

“Wazazi sasa wanafahamu hatari ya kutowapatia chanjo watoto wao dhidi ya polio,” amesema Bi Komba lakini akiongeza kuwa wakati mwingine wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa vijiji pale ambapo familia zinakataa watoto wao kuchanjwa.

Christelle Bangondo, mama wa watoto wawili, amekuwa tayari kuwaleta watoto wake kwa ajili ya kuchanjwa mara tu timu ya usambazaji chanjo ilipofika kijijini kwake akisema anaiamini chanjo baada ya chanjo za awali dhidi ya pepopunda na kikohozi kikali, zilivyowasaidia watoto wake kutopata magonjwa hayo.

Mara ya mwisho kutokea kwa mlipuko mkubwa wa aina hiyo ya polio inayodhibitiwa hivi sasa nchini Jamhuri ya Kongo ulishuhudiwa mwaka 2010. Aina hiyo ya kwanza ya polio kati ya aina tatu, iliwakumba watu 180 na kusababisha vifo vya watu 85 wengi wao wakiwa katika mji wa Pointe Noire na mlipuko huo ulihusishwa na mlipuko wa ugonjwa huo uliokuwa unaendelea katika nchi jirani ya Angola.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud