Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 120,000 wameathirika na mafuriko Madagascar:UNICEF

UNICEF nchini Madagascar inachagiza haki za watoto kupitia michoro
© UNICEF/Abela Ralaivita
UNICEF nchini Madagascar inachagiza haki za watoto kupitia michoro

Watu 120,000 wameathirika na mafuriko Madagascar:UNICEF

Tabianchi na mazingira

Mvua kubwa zilizonyesha kwa wiki mbili zilizopita nchini Madagascar zimeathiri watu 120,000 ikiwakata kabisa na huduma za barabara, kusambaratisha shule 174, na kuwalazimisha watu 16,000 kusalia bila makazi.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis mafuriko hayo hajapewa uzito wa kimataifa au ufadhili , lakini wadau wa kitaifa, serikali na mashirika ya misaada nchini Madagascar wamefanya kila wawezalo wakiwa na rasilimali chache kukabiliana na hali hiyo hasa kukidhi mahitaji ya dharura.

Shirika hilo linasema mafuriko sio hadithi pekee ni mfano mmoja tu wa changamoto lukuki zinazowakabili watoto nchini Madagascar ikiwemo pia majanga ya asili, ukame na maradhi kwa mwaka mzima.

Changamoto hizo zimezidishwa makali na mabadiliko ya tabianchi na zinahitaji jicho na msaada wa kimataifa.

Utafiti wa karibuni nchini hu ambao matokeo yake yatatolewa hivi karibuni UNICEF inasema umeonyesha kwamba hali ya watopto haijaimarika tangu takwimu zingine zilipokusanywa mwaka 2012 na wakati mwingine inakuwa mbaya zaidi.

Hali halisi ya watoto

Kwa mfano kutokana na huduma duni za usafi UNICEf inasema asilimia 40 ya watu nchini humo bado wanajisaidia haja kubwa katika maeneo ya wazi, na athari zake asilimia 93 ya maji ya kunywa katika maeneo ya vijijini yana vijidudu vya E-coli.

Hali hii ikiongezewa na umasikini na lishe dunia imesababisha moja ya hali mbaya zaidi ya utapiamlo duniani ambapo asilimia 42 ya watoto wa chini ya umri wa miaka 5 nchini humo wamedumaa au wana unyafuzi.

Watoto na wanawake waliofurushwa kufuatia kimbunga cha Enawo katika darasa huko Sava, Madagascar. Picha: UNICEF Madagscar (maktaba)
UNICEF
Watoto na wanawake waliofurushwa kufuatia kimbunga cha Enawo katika darasa huko Sava, Madagascar. Picha: UNICEF Madagscar (maktaba)

Nchi hiyo pia inakabiliwa na changamoto kubwa ya elimu, hata kabla ya mafuriko kusambaratisha shule, madarasa 2500 yalikuwa yanahitajika ili kukidhi mahitaji ya idadi ya watu inayokuwa kwa kasi nchini humo.

Lakini utafiri wa karibuni pia unaonyesha kwamba asilimia 7 tu ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 7-14 ndio walio na elimu ya msingu ya kujua kusoma na kuandika.

Chanjo haitoshelezi

Linapokuja suala la afya shirika hilo la kuhudumia watoto linasema watoto chini ya theluthi ndio waliopata chanjo kamili. Na milipuko ya magonjwa ya kila mwaka ya polio na tauni yameathiri uwezo wa mfumo wa afya kuboreka na kuwekeza katika huduma.

Na magonjwa mapya kama milipuko ya surua mwaka huu ambayo ilikatilia maisha ya watoto 1200 vinazidi kudidimiza mfumo wa afya.

Changamoto nyingine ni kwamba wasichana wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18. Na ajira kwa watoto imeshamiri Zaidi ya theluthi moja ya watoto wakichukuliwa kufanya kazi katika mazingira ya hatari kama vile kwenye mgodi wa mica.

Madagascar ina jumla ya watu milioni 25 na nusu yake ni watoto na zaidi ya robo tatu ya watoto hao wanaishi katika ufukara na hatari kubwa.

Ingawa UNICEF na washirika wake wanafanya kila wawezalo kukidhi mahitaji ya watoto nchini humo lakini kuboresha hali ya watoto Madagascar kunahitaji hatua za muda mrefu na endelevu na msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa sio tu wakati wa majanga na milipuko ya magonjwa .

Wasiwasahau watoto wa Madagascar, wanahitaji hadithi zao kuelezwa, wanahitaji msaada wa kimataifa na wanahitaji msaada wa muda mrefu limesema shirika la UNICEF.