Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bachelet na Uganda watia saini makubaliano mapya kuhusu ofisi ya haki za binadamu

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Bachelet na Uganda watia saini makubaliano mapya kuhusu ofisi ya haki za binadamu

Haki za binadamu

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet na serikali ya Uganda wametia saini makubaliano mapya ya kuendelea kuwepo kwa ofisi ya haki za binadamu nchini humo kwa miaka mingine mitatu.

Makubaliano hayo yalitiwa saini Jumapili baina Kamishina huyo Bi. Bachelet na waziri wa mambo ya nje wa Uganda, Sam K. Kutesa, kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa Muungano wa Afrika AU, mjini Addis Ababa Ethiopia.

Muafaya huo utahakikisha kuendelea kuwepo na kufanya kazi kwa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Uganda ambapo sasa ni miaka 14 tangu ilipoanzishwa.

Kamishina mkuu amesema kumekuwa na hatua zilizopigwa kwa miaka hiyo 14, lakini ofisi yake sasa iko tayari kuendelea kuisaidia Uganda katika maeneo ya haki za binadamu ambayo hatua bado zinahitajika.

Chini ya makubaliano hayo mapya ofisi ya Haki za binadamu Uganda itakuwa na majukumu mbalimbali ikiwemo Mosi kuishauri na kuisaidia serikali ya Uganda kuhusu sera, mipango na hatua kwa ajili ya kuchagiza na kulinda haki za binadamu Uganda, pili kuimarisha taasisi za haki za binadamu, asasi za kiraia na wadau wengine kuchagiza na kulinda haki za binadamu, tatu shauri na kuisaidia tume ya haki za binadamu nchini Uganda katika kutekeleza kanuni za kimataifa za haki za binadamu, viwango vya kimataifa na matokeo ya mikakati ya haki za binadamu.

Nne amesema ni kufuatilia hali ya haki za binadamu nchini Uganda kwa ushirikiano na tume ya haki za binadamu ya nchi hiyo.

Na tano kutoa shughuli za mafunzo kuhusu mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu kwa maafisa wa serikali wa sekta husika na pande zingine katika kanda pamoja na taasisi za kitaifa za haki za binadamu na mashirika ya asasi za kiraia.