Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miji inapaswa kuwa kwenye moyo wa maendeleo endelevu-Antonio Guterres

Mji unaoelea kama ulivyobuniwa na Oceanix
Picha kutoka video ya Oceanix
Mji unaoelea kama ulivyobuniwa na Oceanix

Miji inapaswa kuwa kwenye moyo wa maendeleo endelevu-Antonio Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Ufunguzi rasmi wa Kikao cha 10 cha Jukwaa la miji (WUF) umefanyika mjini Abu Dhabi,UEA leo jumapili, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia ujumbe wake wa video amewaambia wajumbe kuwa majiji na miji ni muhimu kuleta maendeleo endelevu kote ulimwenguni katika kipindi cha miaka kumi ijayo.

Aidha Katibu Mkuu Guterres ameushukuru uongozi wa Abu Dhabi kuwa mwenyeji wa mkutano huu ambao kwa mara ya kwanza unafanyika katika ukanda huo wa Uarabuni.

"Tunapouanza muongo wa kuchukua hatua za kufanikisha Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, majiji na miji na jamii vitakuwa moyo wa kazi hii. Umoja wa Mataifa unawategemea viongozi wa chini na wa kitaifa, biashara, asasi za kijamii na wadau wengine kusaidia kutoa suluhishokwa matishio ya dunia ikiwemo dharura ya mabadiliko ya tabianchi.” Amesisitiza Bwana Guterres katika ufunguzi huo ambao umefanyika kwa sherehe kubwa ambazo zimetawaliwa na mfumo wa hali ya juu wa teknolojia.

Jukwaa limefunguliwa rasmi na Sheikh Theyab Mohammed bin Zayed Al Nahyan, mwanamfalme wa Abu Dhabi akiambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na makazi UN Habitat, Maimuna Mohd Sharif.

Mkurugenzi huyo wa UN-Habitat amewaambia wana jukwaa kwamba, “ninachotegemea kukiona kutoka kwenye kikao cha kumi ni maamuzi kuhusu hatua zitakazochukuliwa. Ahadi ambazo zitafanywa chini ya kujitolea kwa mtu mmoja mmoja, jamii, majiji n anchi, kitaifa na hata kikanda, pamoja na ngazi ya kimataifa kusaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu kufikia mwaka 2030.”

Tweet URL

 

Wazungumzaji katika mkutano huo wamuuunga mkono Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat kuwa ni muhimu Jukwaa hili lije na hatua thabiti.

Jukwaa hilo linazikutanisha zaidi ya nchi 160 ili kutafuta namna ya kushughulikia masuala muhimu ya ukuaji wa miji ambao zaidi ya washiriki 18,000 waliojiandikisha na wazungumzaji 580, watu 133 wakishiriki kwa kuonesha miradi na bidhaa mbalimbali, wote kwa siku sita watakuwa wakitafuta namna bora ya kuwa na miji bora ya siku za usoni.