Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atoa wito wa mshikamano kupambana na changamoto zinazoikabili Afrika

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia Mkutano wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia, 09 Februari 2020
UNECA
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia Mkutano wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia, 09 Februari 2020

Katibu Mkuu wa UN atoa wito wa mshikamano kupambana na changamoto zinazoikabili Afrika

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo jumapili ameuambia Mkutano wa Muungano wa Afrika unaowakutanisha wakuu wa serikali za barani Afrika kuwa changamoto zinazoyakabili mataifa ya Kiafrika ni "ngumu, zilizo na malengo mbalimbali na zinazofika mbali” lakini mwitikio wa pamoja, kamilifu na ulioratibiwa na jumuiya ya kimataifa.

Katibu Mkuu Guterres ameuambia mkutano huo unaofanyika kila mwaka ukikutanisha mataifa 55 ya Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kwamba ushirikiano wa kimkakati kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU, ni "muhimu sana" na ana uhakika kwamba changamoto za Afrika zinaweza kutatuliwa kupitia uongozi wa Afrika.

Changamoto za Afrika

Bwana Guterres ameyataja baadhi ya matatizo makubwa yanayolikabili bara la Afrika akianza na umaskini ambao amesema kuna haja ya kupambana nao kupitia muongo wa kuchukua hatua kuelekea kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs ambayo yanaenda na Ajenda ya Afrika ya mwaka 2063.

Aidha amesema mataifa ya Afrika yanafanyia kazi suala la ufisadi, kuboresha mifumo ya kodi, utawala na taasisi, lakini kwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kusaidia juhudi hizi kwa mkakati imara zaidi ikiwemo kupambana na mtiririko wa fedha haramu.

Bwana Guterres pia amesisitiza suala la usawa wa kijinsia akisema ni muhimu na kwamba, “amani, mshikamano wa kijamii na maendeleo endelevu, vinahitaji mchango na uongozi wa wanawake.”

Vilevile amesisitiza kuwahusisha na kuwawezesha vijana akisema kuwa hilo ni suala muhimu kisha akaongeza, “nimetiwa moyo na vijana barani Afrika ambao wamekuwa watetezi wa amani kupitia mazungumzo na kushughulikia sababu za mizozo.”

Tweet URL

 

Mabadiliko ya tabianchi

Akigeukia upande wa mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaambia wakuu wa serikali za barani Afrika kuwa bara la Afrika lina mchango mdogo kabisa katika kusababisha mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kuongezeka kwa joto duniani, lakini bara hili ni moja ya sehemu za mwanzo kudhurika.”

Katibu Mkuu ameupongeza uongozi wa Afrika kwa "uongozi wa maadili na siasa ya muda mrefu kuhusu dharura ya mabadiliko ya tabianchi."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na wakuu wa nchi wakati wa Mkutano Mkuu wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, 09 Februari 2020
UNECA
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na wakuu wa nchi wakati wa Mkutano Mkuu wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, 09 Februari 2020

 

Kunyamazisha bunduki ili kupambana na ugaidi pamoja

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza mafanikio ya ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kupitia mpango wa "Kunyamazisha Bunduki", akisema juhudi za pamoja zimeendeleza amani, hasa katika miezi michache iliyopita katika mabadiliko ya utawala wa kidemokrasia nchini Sudani.

"Tunazidi kuhitaji operesheni za amani na kupambana na magaidi zinazotekelezwa na Muungano wa Afrika na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.” Amesisitiza.