Jukwaa la kimataifa la miji linaonekana kutambua ‘maono ya pamoja’ kuhusu miji ya siku za usoni
Jukwaa la kimataifa la miji linaonekana kutambua ‘maono ya pamoja’ kuhusu miji ya siku za usoni
Kikao cha kumi cha Jukwaa la Kimataifa la miji, WUF10, mkusanyiko mkubwa zaidi wa dunia kuhusu miji ya siku zijazo, umeanza jumamosi hii mjini Abu Dhabi, mji mkuu wa muungano wa nchi za UAE ambako maelfu ya watu wanashiriki katika majadiliano, kupitia mikusanyiko tofautitofauti inayowakilisha vijana, wanawake, jamii za mashinani, serikali za kitaifa na kikanda pamoja biashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la makazi la Umoja wa Mataifa, UN-Habitat, Maimunah Mohd Sharif amewasihi washiriki wa mkusanyiko huo kuzingatia na kujikita katika matokeo halisi.
“Ninatambua kuwa tuna maono ya pamoja kuhusu miji endelevu na salama. Tutaenda mbele zaidi leo. Tunafahamu kuwa ukuaji wa miji hauzuiliki.” Amesisitiza Bi Sharif katika tukio la kwanza la mkutano wa siku sita ambao unafanyika kwa mara ya kwanza katika ukanda wa uarabuni.
‘Hakuna muda uliosalia’
Mkutano wa vijana umewakilishwa kwenye kusanyiko la ufunguzi na Leah Namugerwa mwenye umri wa miaka 15 ambaye ni mwanaharakati kutoka Uganda ambaye amewaeleza washiriki kuwa ni “ni wazuri katika mipango lakini si katika utekelezaji.”
“Niko hapa kuhamasisha hatua kuhakikisha kuwa watoto na vijana wanawakilishwa ipasavyo katika michakato ya maamuzi. Tunatakiwa kuchukua hatua. Hakuna muda uliosalia…tafadhalini chukueni hatua dhidi ya mabadiliko hivi sasa.” Amesihi.
‘Vijana wana jukumu kubwa’
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Mazingiwa wa Umoja wa Mataifa UNEP, Joyce Msuya ameuambia mkutano wa vijana kuwa, “Vijana wana jukumu kubwa la kuendesha utashi wa kisiasa. Ni wakati sasa wa kuwaamini vijana. Wako tayari kusikiliza, kuunganisha, kujifunza na kuongoza.”
Naye kiongozi wa kijamii mdogo kutoka Kenya Isaac Muasa ameuambia mkutano wa vijana kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa ajira na fursa.