Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzunguko wa kwanza wa mazungumzo ya kijeshi kuhusu Libya wakamilika Geneva Uswisi

Matokeo ya shambulio la kituo cha kizuizini cha Tajoura mjini Tripoli, Libya Julai 2.
IOM/Moad Laswed
Matokeo ya shambulio la kituo cha kizuizini cha Tajoura mjini Tripoli, Libya Julai 2.

Mzunguko wa kwanza wa mazungumzo ya kijeshi kuhusu Libya wakamilika Geneva Uswisi

Amani na Usalama

Mzunguko wa kwanza wa mazungumzo ya Kamisheni ya Pamoja ya kijeshi au 5 + 5, ambayo yalianza Jumatatu 3 ya mwezi huu wa Februari 2020, umehitimishwa leo hii alasiri katika jengo la Umoja wa Mataifa Palais des Nations huko, Geneva Uswisi katika tukio lililohudhuriwa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dkt Ghassan Salamé ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL.

Kutokana na kukamilika kwa mzunguko huu wa kwanza ambayo yalihusisha uapnde wa jeshi la serikali na majeshi yanayoipinga serikali, UNSMIL imetoa shukrani zake kwa pande zote zilizokutana mjini Geneva na kushikilia kwa dhati majukumu waliyokabidhiwa. 

UNSMIL imesema inazingatia makubaliano yaliyopo kwa sasa na umuhimu wa kudumisha usitishwaji mapigano uliotangazwa mnamo tarehe 12 Januari mwaka huu, kuhusu umuhimu wa kuyaheshimu makubaliano hayo na kukataa kuyakiuka.

Aidha UNSMIL imebainisha makubaliano kati y apande zote mbili kuhusu uharaka wa watu wa Libya kulinda uhuru na uadilifu wa nchi yao, kalinda mipaka, kulinda mchakato wa kitaifa wa maamuzi na uingiliaji wa mataifa ya nje katika mgogoro na pia kuzuia kutoka kwenye mataifa mengine na kuwafukuza ndani ya nchi na wakati huo huo wakiendelea kupambana na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda, ISIS na Ansar al-Sharia.

Pande zote mbili katika mazungumzo zimeonesha kuunga mkono mpango wa kubadilishana wafungwa, kurejesha miili ya waliopoteza maisha na pia kukaribisha usaidizi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika mchakato huo wakati wowote mahitaji yanapotokea.

Hata hivyo taarifa hiyo ya UNSMIL imeeleza kuwa, “ijapokuwa pande zote mbili zimekubaliana kuhusu hitaji la kuharakisha kurudi kwa watu waliofurushwa katika makazi yao na kujikuta wamekuwa wakimbizi wa ndani, IDPs, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano, hakukuwa na makubaliano kamili kuhusu namna nzuri ya kuweza kurejesha hali nzuri katika maeneo hayo.”

Pande zote mbili zimekubaliana kuendelea na mazungumzo ili kufikia makubaliano kamili ya usitishaji silaha ambapo UNSMIL imependekeza mzunguko wa pili wa mazungumzo uwe tarehe 18 Februari mwaka huu hapo hapo mjini Geneva Uswisi.