Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kitabu kinachoeleza mchango wa mwanamke katika usimamizi wa amani chaziduliwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika Uzinduzi wa Kitabu
UN Photo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika Uzinduzi wa Kitabu

Kitabu kinachoeleza mchango wa mwanamke katika usimamizi wa amani chaziduliwa

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewashukuru wanawake wa Afrika kwa ushiriki wao katika ulinzi na ustawishaji wa amani.

Katibu Mkuu Guterres ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kitabu cha “She Stands for Peace”, uzinduzi ambao umefanyika mjini Addis Ababa Ethiopia kandoni mwa Mkutano wa Mwaka wa wakuu wa nchi zinazounda Muungano wa Afrika.

Bwana Guterres akitambua mchango wa wanawake katika hatua iliyofikiwa, amesema miaka ishirini iliyopita, shukrani ziende kwa utetezi wa wanawake wajenzi wa amani hususani wale wa bara la Afrika ambapo kutokana na utetezi au harakati zao Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 1325 kuhusu Wanawake, Amani na Usalama.

“Wakati huo ndio ulikuwa kwa mara ya kwanza wanawake walitambuliwa si kama waathirika wa vita bali pia watu ambao wana taasisi yao na utaalamu, ambao ni mali muhimu ya kupata suluhisho la amani dhidi ya mgogoro.” Ameeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Tweet URL

 

Bwana Guterres ameeleza kuwa tangu wakati huo yaani kati ya mwaka 1990 na 2016 kumekuwa na ongezeko la makubaliano ya amani ambayo yanajumuisha wanawake kutoka wastani wa asilimia 12 kati yam waka 1990 na 2000 hadi asilimia 32 kufikia mwaka 2015.

Lakini Bwana Guterres ameeleza kuwa kwa masikitiko, hali hii ya ongezeko imeshuka kwa kasi ambapo ametoa mfano kwa mwaka 2018 ni makubaliano 4 kati ya 54 ambayo yalikuwa na vifungu vya jinsia, hiyo ikiwa ni chini ya zaidi ya asilimia 8.

Bwana Guterres amekumbushia ambacho alikuwa amekieleza katika mkutano mwingine asubuhi wa ngazi ya juu kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake barani Afrika, kwamba wanawaume ni wagumu kuachia mamlaka na hapo akawaeleza wanawake kuwa mamlaka hayatolewi kirahisi, bali yanatakiwa kuchukuliwa.

Kitabu hiki kimechapishwa kwa ushirikiano wa karibu na kamisheni ya Muungano wa Afrika na kinahusisha idadi kubwa ya wanawake tofautitofauti: kutoka vijiji na mijini; kutoka malezi au maisha bora na kutoka hali duni au hohehahe.

Bwana Guterres amesema, “tunahitajika kufanya zaidi. Kwa mfano tunahitaji maraisi wanawake wengi zaidi, wabunge, mameneja na wakurugenzi.”

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuhusiana na hilo anajivunia kwamba Umoja wa Mataifa tayari umeanza kulifanyia kazi suala hilo kwani wamefikia usawa wa kijinsia katika uongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa katika historia ya miaka 75 ya shirika hilo.

"Kama wanawake wengi katika kitabu hiki, tuna wanawake bora wenye utaalam mkubwa, ambao watasaidia kuongoza Shirika kupitia changamoto za ulimwengu na siku za usoni.” Amehitimisha Bwana Guterres akisikilizwa na wanawake waliohudhuria tukio hilo kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.