Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo dume Afrika bado ni kikwazo kama kwingineko duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia mkutano wa ngazi ya juu wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake barani Afrika
Daniel Getachew/UN Photo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia mkutano wa ngazi ya juu wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake barani Afrika

Mfumo dume Afrika bado ni kikwazo kama kwingineko duniani

Wanawake

Miaka 25 tangu kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa wanawake huko Beijing, China bado mfumo dume umeendelea kuwa kandamizi na kuengua wanawake katika mifumo ya kiuchumi , kijamii na kisiasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo leo huko Addis Ababa nchini Ethiopia ambako anashiriki mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Muungano wa Afrika, AU.

Akizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake barani Afrika, Guterres amesema, mkutano wa Beijing ulikuwa muhimu sana katika kutambua haki za wanawake na watoto wa kike akisema kuwa hadi sasa wanawake wamekuwa nguzo katika kusongesha azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake katika amani na usalama lililopitishwa miongo miwili iliyopita.

Amesema miongoni mwa wanawake walio mstari wa mbele mchango wao umetambuliwa katika kitabu kiitwacho She Stands for Peace yaani anasimamia amani, kutokana na mchango wao kwenye kusaka amani.

Tweet URL

 

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa asilimia 75 kwa wanawake kwenye mabunge barani Afrika, wasichana wengi zaidi kupata elimu na huduma za afya na  hata wanawake wengi zaidi kuliko wanaume barani Afrika kushiriki katika ujasiriamali kuliko eneo lingine lolote duniani.

Hata hivyo amesema mafanikio yaliyopatikana bado hayajaweze kufikia ahadi zilizopitishwa Beijing mwaka 1995.

"Hebu tuwe wakweli, barani Afrika, kama ilivyo katika dunia yote, tunaishi katika mfumo dume uliotawaliwa na tamaduni za kupatia kipaumbele wanaume. Hii bila shaka ni suala la madaraka. Kile nilichojifunza tangu nikiwa mvulana ni kwamba madaraka hupatiwi bali ni lazima yapokwe.”

Amesema na kama ilivyo suala la madaraka kama alivyoelezewa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Moussa Faki“usawa katika vyombo vya maamuzi ni muhimu sana. Na nina furaha kusema kuwa tunafuata mfano huo katika AU na naweza kutangaza kuwa tangu mwezi Januari tumekuwa kwa mara ya kwanza na UN yenye uwiano wa usawa wa kijinsia kwenye ngazi ya viongozi waandamizi.”

Mwanamke ndiye taswira ya umaskini Afrika

Amegusia pia suala la umaskini barani Afrika kubeba taswira ya mwanamke akisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa kwa kila wanaume 100 hohehahe katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 35, wanawake hohehe ni 127 akimaanisha kuwa idadi ya wanawake hohehahe ni kubwa kuliko ile ya wanaume.

Guterres amesema, “wanawake mara nyingi wamejikuta katika ajira zisizo na hadhi na mshahara kiduchu na wanafanya kazi za nyumbani zisizo na ujira.”

Ukatili dhidi ya wanawake bado umeshamiri

Amezungumzia pia suala la ukatili dhidi ya wanawake akisema kuwa bado limeota mizizi, ukatili ambao amesema unashamirishwa na ghasia na mizozo pamoja na ukimbizi.

Katibu Mkuu amesema wakati huu ambapo dunia inaahidi ukpya kufanikisha maendeleo kuelekea usawa wa kijinsia, “nahamasisha nchi za Afrika kwa ubia na mashirika ya kiraia na wadau wengine wachangie katika hatua za yale yalipitishwa Beijing na utekelezaji wake sasa inapotimiza miaka 23 au Beijing+25.”

Amesema kuwa hatua za ubia kufanikisha maazimio ya Beijing zitajenga mafanikio na kufanikisha ahadi za muongo wa mwanamke wa Afrika unaotamatishwa mwaka huu wa 2020.

Mtandao wa wanawake viongozi Afrika.

Katibu Mkuu huyo wa UN ametumia pia mkutano huo kupongeza kuenea kwa mtandao wa viongozi wanawake barani Afrika, akisema kuwa “kuwepo kwa mtandao huu katika ngazi za kitaifa kunachochea ahadi ya kuchechemua harakati za wanawake ambazo ni muhimu katika kuleta mabadiliko ya jamii za Afrika ili ziwe bora zaidi.”

Ni kwa kuzingatia hilo, Katibu Mkuu amesema ni lazima kutumia fursa hizo kujenga usawa wa kijinsia na kuhakikisha kuwa mahitaji ya wanawake na watoto wa kike yanajumuishwa kwa kina katika harakati za kujenga jamii zenye amani, haki na jumuishi.