Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO kuimarisha utafiti na uvumbuzi kwa ajili ya kukabiliana nan virusi vya corona

Watu wakiwa wamevalia vifaa vya kinga uwanja wa ndege wa Chengdu Shuangliu  nchini China.
UN News/Jing Zhang
Watu wakiwa wamevalia vifaa vya kinga uwanja wa ndege wa Chengdu Shuangliu nchini China.

WHO kuimarisha utafiti na uvumbuzi kwa ajili ya kukabiliana nan virusi vya corona

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO imeandaa kongamano wa kimataifa wa utafiti na uvumbuzi kuchagiza hatua za kimataifa kukabiliana na virusi vipya vya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, "kuweka nguvu ya sayansi ni muhimu kwa ajili ya kudhibiti mlipuko huu." Ameongeza kwamba, "kuna maswali yanahitaji majibu, na vifaa tunahitaji kuandaliwa haraka iwezekanavyo."

WHO inachukua jukumu muhimu la kuratibu kwa kuleta jamii ya kisayansi pamoja ili kubaini vipaumbele vya utafiti na kuongeza kasi ya maendeleo."

WHO imetoa taarifa ya kufanyika kwa kongamano hilo mnamo Februari 11-12 jijini Geneva wakati huu ambapo visa vya maambukizi ya virusi vya corona ni 28,060 nchini China na vifo 564. Na nje ya China kuna visa 225 katika nchi 24 na kifo kimoja nchini Ufilipino.

Kongamano hilo litawaleta pamoja wadau muhimu ikiwa ni pamoja na wanasayansi wanaoongoza pamoja na mashirika ya afya ya umma, wizara za afya na wafadhili wanaofuatilia utafiti wa afya ya wanyama wa  virusi vipya vya corona 2019-nCoV na maendeleo ya chanjo, matibabu na utambuzi, miongoni mwa uvumbuzi mwingine.

Washiriki watajadili maeneo kadhaa ya utafiti, pamoja na kutambua chanzo cha virusi na vile vile kubadilishana sampuli za kibiolojia na mundo wa vinasaba.

Wataalam wataendeleza utafiti uliopo wa homa ya mafua ya SARS na  homa ya Mashariki ya Kati ya Corona Mers coronavirus kwa ajili ya kuchunguza mapungufu ya taarifa na vipaumbele vya utafiti ili kuharakisha taarifa za kisayansi na vifaa vya matibabu vinavyohitajika sana kupunguza athari za mlipuko virusi vya corona.

Hatua hiyo itasaidia katika  kuharakisha maendeleo na tathmini kwa ajili ya uchunguzi bora, chanjo na dawa, wakati ukiweka mifumo kuwezesha  upatikanaji wa huduma kwa bei rahisi kwa idadi ya watu walioko hatarini na kuwezesha ushiriki wa jamii.