Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tangu nimeacha ungariba nimeshawaokoa watoto takribani 150-Aliyeacha ungariba

Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.
UNICEF/Holt
Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.

Tangu nimeacha ungariba nimeshawaokoa watoto takribani 150-Aliyeacha ungariba

Wanawake

Tukisalia katika suala hilo la maadhimisho ya siku ya kutokomeza ukeketaji hii leo shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu UNFPA limefanya kongamano ambalo limewakutanisha jijini Dar es Salaam wadau mbalimbali ili kujadili namna bora ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji.

Wadau mbalimbali wakiwemo waliokeketwa, walionusurika, watetezi wa haki na hata mangariba wamehudhuria tukio hilo.

Miongoni mwa waliohudhuria ni manusura Robi Samuel wa ukeketaji ambaye ameanzisha kituo cha Matumaini nyumba salama mkoani Mara ili kupambana na ukatili huo, kituo ambacho tayari kimeshawaokoa watoto 1807. Anaikumbuka siku aliyokeketwa

(Sauti ya Robi)

"Nilikuwa na umri wa miaka 13 baada ya kumaliza darasa la 7. Ndipo mamangu aliniambia, 'Robi inabidi ukeketwe'. Kwa kweli nilikeketwa, na nilipitia katika hali ngumu ambayo nilitoka damu nyingi, nikapoteza fahamu kwa muda mrefu. Hali ambayo ilipelekea hapa ndugu na jamaa kuona kwamba nimekufa. Lakini baadaye niliweza kuzinduka baada ya masaa kama manne matano, na tangu siku hiyo ikawa ni historia kwa familia yangu kuwacha mila ya ukeketaji."

Mshiriki mwingine wa tukio la leo ni Mama Muhabe Marwa kutoka Mgumu Serengeti ambaye kwa miaka mingi alifanya kazi ya ungariba lakini baada ya kuelimika ameacha kazi hiyo. Anasema ameshawaokoa watoto wengi na ingawa anapata changamoto nyingi katika jamii lakini hayuko tayari kurejea katika shughuli za ukeketaji

 (Sauti ya Mama Muhabe)

"Kwa kweli changamoto zipo nyingi sana unazokumbana nazo kwa sababu pale wazee wa mila, kuna vitu mbalimbal ambazo wanaweza kuwa wanakuambia mfanye, na vingine unaona kwako inaumiza sana. Unakuta wanakuita kuenda kukaa nao mkutano wa kujadili namna ya kuanza kazi ya ukeketaji. Na kwa kweli ngariba usipokuwa makini nao, wataweza wakakuua muda wowote. Changamoto ninazokutana nazo ni nyingi sana kutengwa na jamii na ndugu na marafiki. Sasa hivi mimi kwa kweli ni mwanaharakati na Robi Samuel ndio ndugu yangu, ndio amenisaidia. kwa kweli nimeweza kuokoa watoto  150."