Mkakati wa kimatifa wazinduliwa kuhakikisha usalama dhidi ya ugaidi

3 Februari 2020

Wawakilishi kutoka vyama vya michezo vya kimataifa na sekta binafsi wameungana na mabalozi kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Jumatatu ili kuzindua mkakati wa kimataifa  wenye lengo la kulinda hafla kuu za michezo dhidi ya vitisho vinavyohusiana na ugaidi

Mpango huo wa miaka mingi unaangazia maadili mazuri ambayo michezo inakuza kwa ajili ya kusaidia kupingana na kuenea kwa msimamo mkali, haswa miongoni mwa vijana.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi, UNOCT, Vladimir Voronkov amesema, “michezo inasukuma watu kuwa bora, na kulenga juu na zaidi. Inakuza uvumilivu na usawa wa kijinsia. Inaziimarisha jamii, inaimarisha uvumilivu na njia za asili za ushindani kwa mwenendo unayofaa.”

Bwana Voronkov ameongeza kwamba, "michezo ni dhamana ya msingi na ya kweli ya mwanadamu na ni chanjo kali dhidi ya ugonjwa wa uhalifu. Tuna jukumu la kimaadili la kulinda na kukuza michezo."

Kubadilishana uzoefu na taarifa 

Licha ya uwezo wa kuunganisha watu, hafla za michezo zimeghubikwa na mashambulio mabaya ya kigaidi. Mashindano ya Olimpiki ya 1972 na 1996, na, hivi karibuni zaidi, mbio za marathoni huko Sri Lanka na Marekani, ni mifano ya matukio mabaya yaliyofanyika.

Programu hiyo ya kimataifa itaunda miongozo ya kuongeza ushirikiano wa kimataifa, na ushirikiano wa sekta za umma na binafsi, ili kufanya hafla za michezo kuwa salama kwa wachezaji na umma.

Uzinduzi huo utafuatiwa na mkutano wa wataalamu wa siku mbili. Mkutano mwingine unaolenga vijana utafanyika Aprili. Washiriki waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na wawakilishi kutoka Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), kamati mbali mbali za kitaifa za Olimpiki, chama cha kimataifa cha mpira wa miguu, FIFA, na kampuni binafsi.

"Bwana Voronkov ameongeza kwamba, "Kulinda hafla kuu za michezo kunajumuisha ushirikiano na uratibu, pamoja na usalama na mpangilio wa sera muhimu pamoja na kulinda maeneo, usalama mitandaoni, mipango na usimamizi kuhusu migogoro na mawasiliano ya kimkakati.”

 Mkuu huyo wa UNOCT amesema, "kupitia programu yetu ya pamoja, tutaangazia kubadilishana taarifa na uzoefu, kugawana rasilimali na kufanikisha ushirikiano."

Ni muhimu kuendeleza ujumuishaji wa michezo katika mikakati ya maendeleo na amani, kulingana na afisa mkuu wa jukwaa la Umoja wa Mataifa ambalo linakuza mazungumzo ya kitamaduni, uelewa na ushirikiano.

Kwa upande wake mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya muungano wa ustaarabu, UNAOC Miguel Moratinos amesema, "Kwa kweli, michezo inaunganisha na kuponya.” Ameongeza kuwa, "Pia ni lugha ya ulimwengu ambayo wote wawili, mashabiki na wachezaji wanaelewa. Kwa hivyo, wacha wote tuwekeze uwezo kamili wa michezo, na vijana moyoni mwake, kama mchagizaji wa amani na mabadiliko ya kijamii."

Msaada muhimu kutoka Qatar

Qatar, mwenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA la 2022, ni muungaji mkono muhimu wa mpango huo, pamoja na China na Jamhuri ya Korea.

Nchi hiyo  na ofisi ya kupambana na ugaidi ya Umoja wa Mataifa walitia saini makubaliano mwaka jana ya kuanzisha kituo cha kwanza cha ulimwengu cha kutafiti wa mizizi ya tabia ya misimamo mikali kupindukia inayochochea ugaidi.

Katibu Mkuu wa kamati ya maandalizi ya Kombe la Dunia amesema Qatar inachukua hatua katika ngazi ya kitaifa na ya kimataifa ili kuhakikisha usalama katika "mashindano ya kwanza ya michezo ya ukanda huo"

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter