Mzunguko wa umasikini unawaghubika watu wa asili na makabila:ILO

3 Februari 2020

Watu wa asili na wa jamii za makabila wanakabiliwa na umasikini uliokithiri mara tatu zaidi yaw engine huku wanawake kila wakati wakishikilia mkia katika kila Nyanja ya kijamii na kiuchumi kwa mujibu wa wataalam wa shirika la kazi duniani ILO.

Ripoti iliyotolewa leo Jumatatu na wataalam hao wa ILO ina takwimu mpya zinazoonyesha kwamba kuna idadi kubwa ya watu wa asili wanaoishi kwa chini ya dola 1.90 kwa siku  wakiwa ni asilimia 18.2 ikilinganishwa na asilimia 6.8 ya watu ambao sio wa jamii za asili.

Shirika la ILo limesisitiza kwamba “mamilioni ya watu wa jamii za asili wamebakizwa nyuma na mzunguko wa umasikini”

Ukubwa wa tatizo

Ripotoi hiyo ya ILO inasema hili ni tatizo kubwa linalohitaji hatua za kimataifa kwa sababu watu hawa walio hatarini idadi yao ni kubwa kuliko ilivyokadiriwa hapo awali.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kuna zaidi ya watu wa asili milioni 476 kote duniani nawengi wao wanaishi katika nchi zenye mafanikio zilizoendelea . Na ripoti inasema “wakati huohuo  mkataba pekee wa kimataifa wa kuwalinda watu hawa na haki zao mkataba namba 169 ni dhaifu. Na kati ya nchi wanachama wa ILO 187 ni wanachama 23 pekee ndio waliotia saini mkataba huo kuhusu haki za watu wa asili ikiwa ni miaka 30 tangu kupitishwa kwake. Hii inamaanisha kwamba karibu asilimia 15 tu ya watu wa asili ndio watakaoweza kunufaika na mkataba huo unaojikita katika utekelezaji wa sera na sheria zilizoundwa kukabiliana na uamasikini, ubaguzi na kuchagiza usawa kupitia majadiliano jumuishi na hulka bora.”

Watu wa asili wamejikita katika sekta isiyo rasmi

Ikijikita katika mfumo wa ajira duniani katika kiashiria cha uendeshaji wa Maisha ya kila siku ripoti hiyo imebaini kwamba watu wengi wa asili wamejikita Zaidi katika sekta isiyo rasmi asilimia 20 zaidi ikilinganishwa na wafanyakazi wengine. Na kutokana na takwimu zilizokusanywa kutoka nchi 23 ambazo ni maskani ya Zaidi ya asilimia 80 ya watu wa asili, ripoti hiyo ya ILO imegundua kwamba wanawake kutoka jamii hizo za watu wa asili wanakabiliwa na changamoto kubwa Zaidi.

Ukiacha kwamba wana fursa ndogo zaidi ya kumaliza elimu ya msingi , ni mmoja tu kati ya 4 ndiye anayefanya kazi ya kulipwa ukilinganisha na mwanamke mmoja kati ya wawili ambao si watu wa asili wanaofanyakazi.

Watafiti bia wanatambua kwamba hata kama watu hao wako katika ajira ya malipo watu wa asili wanalipwa asilimia 18 chini ya wafanyakazi wengine.

ILO inasema duniani kote kuna zaidi ya jamii 5000 za watu wa asili katika nchi 90.

Kikanda Amerika ya Kusini na Caribbea ndiko kuliko na idadi kubwa ya jamii za makabila na watu wa asili ambao ni asilimia 8.5 ya watu wote wakiwa ni wengi kuliko hata ifdadi ya watu wote wa Colombia.

Takwimu kutoka nchi tisa za ukanda huo pia zinaonyesha kwamba jamii hizi za watu wa asili ni asilimia 30 ya watu wote masikini wa kupindukia idadi kubwa zaidi kuliko kwingineko duniani.

Hali kwingineko duniani

Ikilinganisha mwenendo huu kwingineko ripoti ya ILO inasema Afrika ambako kuna zaidi ya watu wa asili milioni 77, ikiwa ni asilimia 6 ya watu wote . ni miongoni mwa asilimia 24 ya watu masikini kabisa.

Baran Asia na Pasifiki watu wa asili milioni 335 ni asilimia 7 ya watu wote na karibu asilimia 16 miongoni mwao wanaishi katika ufukara kutokana na takwimu zilizokusanywa kutoka nchi tano.

Amerika ya Kaskazini hali imeelezwa kuwa tofauti kidogo ambao asilimia mbili ya watu wote ni watu wa asili (milioni 7). Na miongoni mwa watu hao Zaidi ya milioni 7 asilimia 3.5 ndio masikini Zaidi katika jamii.

ILO inaamini kwamba mtazamo wa watu wa asili unapaswa kusikilizwa ili kuweza kuweka sera endelevu za haki za kijamii ambazo zimeainishwa kwenye mkataba namba 169. Hii itasaidia kukabiliana na matatizo ambayo yanawakabili watu wa asili ikiwemo umasikini, kutokuwepo kwa usawa, migogoro na mabadiliko ya tabianchi.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter