Mabadiliko ya tabianchi na machafuko vyatumbukiza mamilioni kwenye njaa Sahel:UN

3 Februari 2020

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa imeonya kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na upungufu wa chakula na fursa muhimu za Maisha Katikati mwa sahel imeongezeka sana katika mwaka mmoja uliopita kutokana na changamoto za usalama na mabadiliko ya tabianchi.

Mashirika hayo la mpango wa chakula duniani WFP, la kuhudumia watoto UNICEF na la chakula na kilimo FAO yamesema kwamba hali huenda ikawa mbaya zaidi endapo jumuiya ya kimataifa haitochukua hatua sasa. “Licha ya hali inayoridhisha katika uzalishaji wa kilimo kwa ujumla watu milioni 3.3  wanahitaji msaada wa haraka Sahel ya Kati kwa mujibu wa tathimini ya mfumo wa uhakika wa chakula.”

Wataalam wanakadiria kwamba karibu watu milioni 4.8 Sahel ya Kati watakuwa katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula hasa katika msimu wa muambo unaoanza Juni hadi Agosti 2020 endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa haraka kuzuia hali hiyo.

Chris Nikoi mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati amesema “Tunashuhudia ongezeko kubwa la njaa Sahel ya Kati, idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula imeongezeka mara mbili baada ya msimu wa mavuno badala ya kupungua.Tusipochukua hatua sasa kizazi chote kipo hatarini”  Kwa mujibu wa mashirika hayo maeneo yanayotia wasiwasi zaidi ni Burkina Faso, Mali na Niger ambako vita bna athari zake katika jamii vimekuwa chanzo kikubwa cha kutokuwa na uhakika wa chakula.

Vita , mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha pia vimewafanya maelfu ya watu kufungasha virago katika nchi hizo. Mabadiliko ya tabianchi pia yameelezwa kuchochea hali hiyo na kusababisha mifugo kujikusanya katika eneo moja hali inayotishia kuzuka kwa machafuko baina ya wakulima na wafugaji.

“Tusiposhughulikia mizizi ya mgogoro huu mamilioni ya wafugaji na wakulima wataendelea kuhitaji msaada wa haraka kila mwaka kama ilivyokuwa mwaka 2019 na sasa 2020” amesema Robert Guei mratibu wa Fao katika ukanda huo.

Naye mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati wa UNICEF Marie-Pierre Poirier amesema “Mgogoro Sahel ya Kati ni zahma inayoikumba kanda nzima na kukiweka kizazi chote cha watoto katika hatari. Maelfu ya watoto wanakosa elimu, wako katika hatari ya kunyonywa, na kupata utapiamlo na ndio wanaoendelea kulipa gharama kubwa ya mgogoro ambao hawakuuanzisha. Tunahitaji kuchukua hatua sasa kuepuka janga zaidi”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter