Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha sheria mpya ya Tajikistan inayowapa hadhi wakimbizi na wasio na utaifa

Mtoto akinywa maji katika kambi wilaya ya Khuroson, Tajikistan
UN
Mtoto akinywa maji katika kambi wilaya ya Khuroson, Tajikistan

UNHCR yakaribisha sheria mpya ya Tajikistan inayowapa hadhi wakimbizi na wasio na utaifa

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limekaribisha sheria mpya iliyopitishwa nchini Tajikistan ambayo inaruhusu raia wa kigeni na watu wasio na utaifa wanaoishi nchini humo kuhalalisha ukaaji wao kwa kupata vibali vya kuishi moja kwa moja ambavyo vitawawezesha pia baada ya miaka mitatu kuomba uraia wa Tajikistan.

Kwa mujibu wa UNHCR hatua hiyo ni muhimu katika kuelekea kumaliza tatizo la kutokuwa na utaifa nchini humo. Sheria hiyo ya msamaha iliidhinishwa na rais wa Tajikistan Emomali Rahmon, tarehe 18 Desember 2019 na imeanza kutumika rasmi tarehe 7 Januari 2020.

Mamkala nchini humo inakadiria kwamba sheria hiyo itawanufaisha watu  20,000 raia wa zamani wa Muungano wa Soviet ambao waliingia nchini Tajikistan kabla ya mwisho wa mwaka 2016.

Wanajumuisha raia wa kigeni na watu wasiokuwa na uraia na uhalali wa kuishi nchini humo kisheria ambao sasa wataweza kuhalalisha ukaaji wao nchini humo na wamesamehewa adhabu yoyote ya kuishi nchini humo kinyume cha sheria.

Kaimu mkuu wa operesheni za UNHCR nchini Tajikistan Roza Minasyan amesema “UNHCR inapongeza juhudi za serikali ya Tajikistan kwa kutimiza ahadi yake ya kukomesha hali ya kutokuwa na utaifa. Kupitia sheria ya msamaha watu wenye hali ngumu wataweza kupata vibali halali vya kuishi na hivyo kuwa na haki na kupata huduma “.

Tajikistan imekuwa ikilifanyia kazi suala la kukomesha kutokuwa na utaifa tangu mwaka 2014 na tayari watu 40,000 uraia wao umethibitishwa kupitia mfumo wa kisheria uliopo.

Sheria hiyo mpya pia inatimiza ahadi iliyowekwa na Tajikistan wakati wa mkutano wa ngazi ya juu wa wa kimataifa wa UNHCR kuhusu kutokuwa na utaifa uliofanyika Oktoba mwaka 2019.

TAGS:UNHCR, Tajikistan, kutokuwa na utaifa, wakimbizi