Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO inashirikiana na serikali husika kukabiliana na mlipuko wa nzige wa jangwani pembe ya Afrika

Uvamizi wa nzige unaweza kuathiri uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu.
Photo: FAO/Yasuyoshi Chiba
Uvamizi wa nzige unaweza kuathiri uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu.

FAO inashirikiana na serikali husika kukabiliana na mlipuko wa nzige wa jangwani pembe ya Afrika

Masuala ya UM

Mlipuko wa nzige wa jangwani unaendelea kuwa mbaya na ni tishio kubwa kwa uhakika wa chakula na mbinu za kujipata kipato katika Pembe ya Afrika. 

Hivi sasa Ethiopia, Kenya, na Somalia ndio nchi zilizoathirika zaidi lakini hatari kwa Sudani Kusini na Uganda zinaongezeka limesema Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO.

Kenya ni moja ya nchi ambako nzige hao wamevamia na mazao ya chakula na malisho ya mifugo yanaathiriwa vibaya. Esther Kithuka ni mkulima kaunti ya Kitui

(Sauti ya Esther-Kiswahili)

Nchini Ethiopia, Kenya na Somalia, sehemu kubwa ya idadi ya watu wanategemea kilimo na mifugo kwa maisha yao na karibu watu milioni 12 tayari wako katika hali ya ukosefu wa uhakika wa chakula kutokana na ukame na mafuriko. Bukar Tijani, Naibu Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Ulinzi wa watumiaji FAO anasema

(Sauti ya Tijani)

"Kwa sasa Kenya, Somalia na Ethiopia zimekuwa nchi ambazo zimeshambuliwa na nzige wa Jangwani kwa mabilioni. Lakini pia, kuna nchi zingine zilizo hatarini, hasusan Sudan Kusini, Uganda na Eritrea, ambayo pia imeathiriwa kufikia sasa. Na pia  kando ya bahari Sham, Saudi Arabia na Yemen ambazo tayari zimevamiwa. Na katika ukanda wa mashariki, India, Pakistan, Iran. Nchi hizo zote zimeathirika.”

Kwa upande wake Dominique Burgeon, mkurugenzi wa kitengo cha dharura na ukarabati, FAO anasema

(Sauti ya Burgeon)

"Tuko katika ukanda ambao watu zaidi ya milioni 11 katika nchi hizo tatu tayari wanakabiliwa na kutokuwa na wa uhakika wa chakula. Kwa hivyo, tunahitaji kufanya juhudi zote ili kuzuia kuzorota kwa hali. Tunajua kwamba nzige hawa ambao tunawaona hapa wanaweza kuleta uharibifu mkubwa sio tu katika suala la mazao lakini pia katika suala la malisho na kwa hivyo kuathiri maisha ya jamii za wafugaji. Ili hilo lifanyike, katika wakati huu muhimu, suluhisho la pekee ambalo linafanya kazi ni umwagiliaji wa dawa wa angani. "

FAO kwa kushirikiana na serikali na wadau wake inachangisha fedha kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko katika juhusi za umwagiliaji dawa angani na ardhini.

Na inaonya kuwamba iwapo operesheni za kukabiliana na hali hivi sasa hazitaimarishwa basi huenda nzige hao wakasambaa katika nchi ambako tayari wamevamia, pamoja na nchi zingine.