Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa Trump Mashariki ya Kati unaegemea upande mmoja:Lynk

Julai 12 2018, mvulana wa umri wa miaka 8, Hamid akitizama mji wa kale wa Hebbron kutoka kwa paa la nyumba yake.
UNICEF/Izhiman
Julai 12 2018, mvulana wa umri wa miaka 8, Hamid akitizama mji wa kale wa Hebbron kutoka kwa paa la nyumba yake.

Mpango wa Trump Mashariki ya Kati unaegemea upande mmoja:Lynk

Haki za binadamu

Mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu mzozo wa Israeli na Palestina ni pendekezo linaloegemea kabisa katika upande mmoja kwa mzozo huo, amesema Michael Lynk, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya hali ya haki za binadamu katika eneo la Palestina linalokaliwa tangu mwaka 1967.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Bwana Lynk amesema “Anachokipendekeza Trump ni suluhu ya taifa moja na nusu , na taifa hili kipande linapungukiwa sifa za kawaida zinazoeleweka juu ya haki ya uhuru wa kupeperusha bendera yake na kutengeneza stempu, linaweza kuwa chombo kipya katika sayansi ya kisasa ya kisiasa.

Amesisitiza kwamba hiki sio kichocheo cha haki na amani ya kudumu lakini badala yake ni kuudhinisha uundwaji wa Bantustan Mashariki ya Kati katika karne ya 21.

“Kipande cha taifa la Palestina lililodhaniwa na mpango wa Marekani litakuwa ni visiwa vilivyotawanyika eneo lisilo na umoja likizungukwa kabisa na Israeli, bila kuwa na mipaka ya nje, hakuna udhibiti wa uwanja wake wa ndege, hakuna haki ya kuwa na jeshi kwa kutetea usalama wake, hakuna msingi wa kijiografia wa kuwa na uchumi unaofaa , hakuna uhuru wa kutembea na kukosa uwezo wa kulalamika kwenye jukwaa la kimataifa na mahakama dhidi ya Israeli au Marekani.”

Mwakilishi huyo ameelezea hofu kwamba mpango huo uliotangazwa juma hili na Marekani utakiuka kila msingi wa sheria za kimataifa zinazosimamia mzozo baina ya Israel na Palestina. “Kutotekeleza misingi hiyo ya kisheria kunatishia kusambaratisha muafaka wa muda mrefu wa kimataifa kuhusu mzozo wa Masharikin ya Kati na itakuwa ni kukumbatia siasa badala ya haki, mamlaka baadada ya haki na kudhibiti mgogoro badala ya kusuluhisha mgogoro.”

Sehemu kuu ya mpango huo wa Trump ingeruhusu Israel kudhibiti asilimia 30 ya Ukingo wa Magharibi . Kwa mujibu wa Bwana Lynk “kuhodhi sehemu ya eneo la wengine ni marufuku kwa mujibu wa sheria za kimataifa zilizowekwa kwenye katika ya Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1945.”

Na tangu mwaka 1967 amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza msingi huu dhidi ya ukaliaji wa Israel mara nane na hivi karibuni ilikuwa Desemba 2016 iliposisitiza tena msingi huo ikisema ni ukaliaji wa kimabavu wa eneo hilo.

Mwakilishi huyo ameitaka jumuiya ya kimataifa kulaani vikali mpango huo wa kutoa idhini kwa Israel kuendelea kuhodhi maeneo ya Palestina. “Mpango huu unakiuka haki ya Wapalestina ya kujitawala na unatishia kuurudisha ulimwengu katika zama za kiza ambazo uvamizi ulikuwa unaruhusiwa, mipaka ilikuwa inachorwa upya na uhuru wa mipaka ulikuwa ukikiukwa.”