UNHCR yawajengea nyumba wakimbizi na wenyeji wao nchini Niger

UNHCR imeanzisha programu ya malipo ambayo inawaajiri vijana kutoka katika jamii za wenyeji katika eneo la Awaradi, Niger ili kutengeneza matofali
UNOCHA/Eve Sabbagh
UNHCR imeanzisha programu ya malipo ambayo inawaajiri vijana kutoka katika jamii za wenyeji katika eneo la Awaradi, Niger ili kutengeneza matofali

UNHCR yawajengea nyumba wakimbizi na wenyeji wao nchini Niger

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi amezindua ujenzi wa nyumba zilizojengwa kwa ubunifu nchini Niger kwa lengo la kutatua mahitaji ya kibinadamu ya haraka na yanayoongezeka katika eneo la Sahel wakati suluhisho la kudumu likitafutwa kwa ajili ya wakimbizi na watu wa Niger walioko hatarini.

Ouallam katika mkoa wa Tillabery magharibi mwa Niger, ni eneo mwenyeji wa maelfu ya wakimbizi wa Mali, wengi wao wakiwa ni waliiikimbia nchi yao mwanzoni mwa mapigano mnamo mwaka 2012, pamoja na watu wa Niger wengine ambao walikimbia nyumba zao siku chache zilizopita wakati ukosefu wa usalama ukiendelea.

Kwa kushirikiana na serikali ya Niger, na ufadhili kutoka shirika la maendeleo la Ujerumani GIZ, UNHCR imeanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba imara za kudumu katika maeneo ya mji huo ambazo zitawahudumia wakimbizi na familia za wenyeji zilizoko hatarini. Familia zitapokea hati za umiliki wa nyumba ambazo zinajengwa katika ardhi iliyotolewa na serikali.

Mradi huo pia ni mkakati wa ustawi kwa maisha ya wenyeji na wakimbizi kwani wafanyakazi wanatoka katika pande zote mbili na wanafundishwa kutengeneza matofali ambayo yanatumia simenti kiasi kidogo ikilinganishwa nay ale ya kawaida.

Nyumba 1000 zitajengwa katika mwaka mmoja na nusu ujao kwenye eneo la Ouallam wakati katika mji wa Ayerou nako zitajengwa nyingine 1000 na kule Abala zikijengwa zingine 2000.

Bwana Grandi anasema,“Mpango huu ni kuwaunganisha, zaidi kujumuisha jamii za wakimbizi katika jamii za wenyeji. Na hapa kwasababu ya mafdhila ya wakimbizi wa ndani, wakimbizi wa ndani pia wamejumuishwa. Na hii ndio sababu tuko hapa. Tuko hapa kuzindua nyumba ambazo watapewa wakimbizi na wenyeji, kukuza pia umoja wa kijamiikati ya makundi ambayo yanashirikiana pamoja hapa.”

Takribani wakimbizi 60,000 kutoka Mali wamekuwa wakiishi katika kambi nchini Niger. Na katika wiki za hivi karibuni wenyeji wa Niger nao wamekimbia kutoka katika kiji chao na kuingia Ouallam  na kujikusanya katika kambi ya wakimbizi wa ndani.

Mariam Walate Intanere ni mkimbizi kutoka Mali anasema, "Kupata nyumba hii kutasaidia kulifanya jukumu langu kuwa jepesi. Kutasaidia familia yetu kubakia salama wakati wa msimu wa mvua. Wakati wa msimu wa mvua tulikuwa tunalazimika kujenga tena nyumba ztu kwa miti. Huwezi kulinganisha.”