Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisheni mapigano ya Syria kuepuka ‘janga zaidi la kibinadamu’-OCHA

Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA
UN Photo/Loey Felipe
Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA

Sitisheni mapigano ya Syria kuepuka ‘janga zaidi la kibinadamu’-OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Hali mbaya ya kibinadamu na ambayo inazidi kudorora” inayoathiri wanawake na watoto kaskazini magharibi mwa Syria imekuwa suala kuu kwa Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA, Mark Lowcock ambaye amezungumza na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa  hii leo jumatano mjini New York, Marekani.

“Uadui umeongezeka katika siku za hivi karibuni katika eneo la Idlib hususani katika maeneo ya Ma’arat al-Numan, Saraqeb na magharibi mwa Aleppo. Hali mbaya zaidi tuliyoiona kwa mwaka jana.” Amesema Bwana Lowcock akielezea kuhusu mapigano katika maeneo hayo.

Ameongeza kuwa raia wanaendelea kuwa waathirika wa mabomu na vilipuzi vizito. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR, kwa mwezi huu wa Januari, imerekodi takribani vifo 81 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto waliouawa kutokana na mapigano ya ardhini na angani kati ya tarehe 15 na 23 mwezi huu pekee.

“Jumla hii ni nyongeza katika zaidi ya vifo vya raia 1,500 ambavyo OHCHR imevithibitisha tangu machafuko yalipoanza tena mwezi April mwaka jana 2019.” Amefafanua Lowcock.

Wakati ripoti za kushitusha zinakuja kutoka kusini mwa Idlib, ambako mamia ya mashambulizi ya anga yanayotekelezwa na serikali yanafanyika zaidi, makundi yasiyo ya kiserikali yenye kujihami kwa silaha yanaendelea kurusha makombora katika mji wa Aleppo, kuua na kujeruhi raia wengi.

“Familia nyingi zimehama mara kadhaa” amesema Bwana Lowcock. “Wanafika katika maeneo yanayodhaniwa kuwa salama, kbala ya mabomu kufuata, kwa hivyo wanalazimika kuhama tena.”

‘Sitisheni’

Katikati ya mapigano, mashirika ya kibinadamu yametoa chakula kwa raia zaidi ya milioni 1.4 na huduma za kiafya kuwatibu takribani watu 200,000.

Akiielezea hali ilivyo Bwana Lowcock ameielezea hali ilivyo kuwa watu wanajiona ni waliotelekezwa na dunia.

“Hawaelewi kwa nini Baraza hili linashindwa kusitisha mauaji ya raia ambao wamekwama katika eneo la vita.” Amesisitiza Bwan Lowcock akiongeza kusema, “ujumbe wao kwenu ni ule ule ambayo niliwaeleza wakati nilipozungumza nami tarehe 30 Julai mwaka jana 2019: “Tunaogopa. Tafathalini tusaidie. Sitisheni mapigani.”.

Watu 70,000 wametawanywa kote kaskazini mashariki

Akirejelea kaskazini mashariki mwa Syria, Bwana Lowcock amesema watu 70,000 wamesalia kuwa wakimbizi wa ndani tangu operesheni za kijeshi zilipoanza mwezi Oktoba mwaka uliopita.

“Nyongeza ya watu 90,000 wanaishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.” Amesema kiongozi huyo akieleza kuwa jumla ya watu milioni 1.8 kaskazini mashariki wana uhitaji wa msaada wa kibinadamu.