Mwakilishi wa UN wa vijana awatembelea vijana Sudan Kusini katika kambi ya ulinzi wa raia

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya vijana Jayathma Wickramanayake amewatembelea vijana wakimbizi wa ndani Sudan Kusini wanaoishi katika kambi ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa karibu na mji mkuu Juba na kusikiliza kilio chao.
Katika kambi ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi wa raia inayohoifadhi wakimbizi wa ndani vijana wako katika harakati za za mafunzo na ujasiriliamali ikiwemo shughuli za ususi na mgeni rasmi mwakilishi wa vijana Jayathima anaonyeshwa kwa vitendo ujuzi wa ususi alioupata mmoja wa vijana baada ya kuishi kambini hapo kwa miaka sita.
Kisha anapata fursa ya kuketi na vijana hao kuwasikiliza. Maelfu ya vijana na watoto Sudan kusini wanaishi katika kambi hii baada ya kukimbia machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe yaliyozuka 2013.
Wengi wamezaliwa hapa na hawajawahi kujua maisha mengine yoyote nje ya kambi hii. Makurar Joch ni mwakilishi wa vijana katika kambi hii ya ulinzi wa raia,“Vijana wote hawako kawaida kama unavyowaona sasa, hjususani kama mimi naweza kusema nimeathirika , huwezi kuona kwa macho lakini ni kihisia. Tafadhali japo chagiza fursa za elimu hicho ni kitu kimoja ninachokitilia mkazo , usisahau tafadhali.”
Hata hivyo vijana hawa wana fursa ya kupata chakula, maji na hata elimu kambini hapo tofauti na maelfu wengine, yakiwemo mafunzo ya ufundi mbalimbali yanayoendeshwa na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF kwa ushirikiano na shirika la maendeleo ya wanawake (WAO).
Kituo hicho kinatoa mafunzo ya kompyuta kwa washicha wadogo ambao wana watoto na vijana walioacha shule, lakini pia mafunzo ya ushonaji, upishi, ususi, useremala, mahesabu na kusoma ikiwa ni pamoja na kukabiliana na ukatili wa kijinsia. Hivi sasa kina jumla ya vijana 315 waliojiandikisha katika mafunzo mbalimbali. Jayathima anasema, “Natumai na kutaraji kwamba wazee wataendelea kuwaunga mkono vijana na hasa ushiriki wa wasichana katika program kama hii na natumai kwamba amani itarejea Sudan kusni na kwamba nyote vijana mtaonekana kama waleta amani na mafanikio na sio watekelezaji wa vita.”
Jayathima amekutana pia na wakufunzi na kusikilizachangamoto zinazowakabili wasichana akiwemo Alice Kidden mwenye umri wa miaka 22 anayelea watoto wake wawili peke yake.“Changamoto zinawakabili wanawake zaidi ya wanaume kwa sababu wanawake wengi ni wajane. Ndio wanaohudumia watoto wao , na hawana msaada wowote kutoka nje.”
Asilimia 72 ya watu wote Sudan kusini ni vijana walio na umri wa chini ya miaka 30 na wengi wao hawana ajira au hawawezi kuajiriwa kwa sababu hawana ujuzi. Jayathima ameahidi kuwasilisha kilio chao kwenye Umoja wa Mataifa na yuko Sudan Kusini kwa ziara ya wiki moja.