Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msitie shaka maoni yenu tutayafanyia kazi vijana:Guterres

Katibu Mkuu António Guterres (katikati kushoto) ashiriki katika Mazungumzo ya UN75 na vijana kuhusu mada ya 'Vijana katika Nafasi ya Kutoa Mwelekeo'.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu António Guterres (katikati kushoto) ashiriki katika Mazungumzo ya UN75 na vijana kuhusu mada ya 'Vijana katika Nafasi ya Kutoa Mwelekeo'.

Msitie shaka maoni yenu tutayafanyia kazi vijana:Guterres

Masuala ya UM

Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake , Umoja wa Mataifa umewaalika vijana kutoka kote duniani kushirikia katika majadiliano kuhusu mustakabali wanaoutaka. Mkakati huo umeanza na mazungumzo baina ya kundi la vijana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye amesikiliza masuala yanayowatia changamoto vijana na mapendekezo yao.

Miongoni mwa masuala yanayowatia hofu vijana na kuongelewa na wengi katika mazungumzo hayo ni ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia kutoa taarifa zisizo sahihi kuchagiza machafuko.

Hayo yamewekwa bayana na vijana wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliopewa jina “UN75” unaoendeshwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo kwamba watu wote wanaweza kuchangia mawazo “ili kujenga mustakabali tunaoutaka” na kufafanua jukumu la Umoja wa Mataifa katika ujenzi wa mustakabali huo.

Mazungumzo hayo kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Antonio Guterres na kundi la vijana wanaowakilisha wenzao kwa mamilioni kutoka nchi mbalimbali ndio umekuwa mwanzo wa mpango wa mjadala huo wa kuelekea maadhimisho ya miaka 75 ya kuanz9shwa kwa Umoja wa Mataifa.

“Tuko hapa kusikiliza na kujua jinsi gani ya kuchukua hatua kuhusu matarajio ya watu, matumaiani yao na wasiwasi wao.” Amesema Guterres akifungua rasmi mjadala huo na kuwaomba washiriki  kutomuuliza maswali kwani hilo sio lengo la mkutano huo.

Kisha vijana wakapata fursa ya kutaja madukuduku yao yanayowatia wasiwasi kuanzia demokrasia, ushirikiano wa kimataifa, hatari za kiusalama, kuendelea kushika kasi kwa mabadiliko ya tabianchi, hadi teknolojia kuendelea kuwa na gharama nafuu na kusaidia kusongesha ubinadamu, lakini pia jinsi inavyoingilia uhuru binafsi na inavyotumika kwa masuala ya kitabibu kuliko kuunda Zaidi na Zaidi silaha za maangamizi.

Dunia katika miaka 25 ijayo

Ikiwa inakabiliwa na changamoto zote hizo Guterres amewauliza vijana nini kinapaswa kubadilika ili dunia iwe bora katika miaka 25 ijayo?

Jibu la kwanza limetoka kwa Jahan Rifai kijana aliyehitimu shahada ya mawasiliano nchini Jordan na ambaye amefanya kazi na wakimbizi. Akielezea hali ya Wapalestina na Wasyria amesema “wakimbizi wangepaswa kuweza kurejea katika nchi zao” na kuongeza kuwa na hapo ndipo dunia inapaswa kuwa tumaini moja bila hofu au chuki.

Mshiriki mwingine amejikita na haja ya teknolojia kutoa huduma kwa ubinadamu na si kinyume na “kwa jamii kuwa jumuishi zaidi .”

Pia vijana hao wanafikiria kwamba katika miaka 25 ijayo dunia inapaswa kuwa inashikamana na ushirikiano wa kimataifa, imepunguza pengo la usawa na kuzimba mapengo ya usawa wa kijinsia.

Jukumu la Umoja wa Mataifa

Na kuhusu jukumu linalopaswa kufanywa na Umoja wa Mataifa katika kutetea ushirikiano wa kimataifa, vijana wamesisitiza kwamba “ni lazima kwa shirika hilo kwa ajili ya kujifunza historia nzuri na kuiendeleza na kutoa kipaumbele kwa ushirikiano wa kimataifa, ingawa pia wameelezea haja ya haraka ya kupunguza urasimu ili kuharakisha mchakato huu.”

Akihitimisha Katibu Mkuu amewashukuru vijana kwa ushiriki wao na kuwakaribisha kusalia katika majadiliano haya muhimu ambayo yatasaidia kukabiliana na vikwazo vya kujenga dunia bora.

“Nawahakikishia kwamba kila mlichokizungumza kitatiliwa maanani” Guterres amewaahidi vijana hao akikamilisha mazungumzo yao.

Huu ndio mwanzo wa mjadala wa kimataifa

Majadiliano ya leo yamefungua pazia kwa maelfu ya wengine  na mikutano itafanyika kila mahali kuanzia bungeni na kwenye vyuo vikuu hadi vijijini na kwenye majukwaa.

Lengo ni kusikiliza watu wengi iwezekanavyo, kuwapa fursa ya kutoa maoni yao, kusisitiza kuhusu vipaumbele na kubadilishana taarifa za matumaini na wasiwasi wao. Na maswali matatu ndio yanayomulikwa :watu wanauonaje mustakabali, ni mienendo gani inayotamalaki duniani hivi sasa na jinsi gani ya kudumisha ushirikiano wa kimataifa.