Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yapeleka msaada China kusaidia waathirika wa virusi vya Corona wakiwemo watoto

Vifaa vya kinga ya kukabiliana na mlipuko ya coronavirus vimeandaliwa ili kusafirishwa kutoka ghala la UNICEF nchini Denmark.
UNICEF/Hendrik Hildelbrandt
Vifaa vya kinga ya kukabiliana na mlipuko ya coronavirus vimeandaliwa ili kusafirishwa kutoka ghala la UNICEF nchini Denmark.

UNICEF yapeleka msaada China kusaidia waathirika wa virusi vya Corona wakiwemo watoto

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limepeleka msaada nchini China ili kusaidia kukinga maelfu ya watu wakiwemo watoto dhidi ya kusambaa kwa mlipuko wa virusi vya Corona

Kwa mujibu wa UNICEF vifaa hivyo vilivyowasili leo mjini Shangai, China ni pamoja na vifaa vya kuchuja hewa na mavazi ya kujikinga  kwa ajili ya wahudumu wa afya ambao wanawahudumia waathirika.

Shehena ya msaada huo ya tani 6 imesafirishwa na UNICEF kutoka katika kituo chake cha hifadhi ya kimataifa cha Copenhagen na itapelekwa hadi Wuhan ambako kuna wagonjwa wengi zaidi.

UNICEF inatarajia kupeleka msaada zaidi katika siku na wiki zijazo. Akisisitiza umuhimu wa msaada huo mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema “Virusi vya Corona vinasambaa kwa kasi kubwa na ni muhimu kukusanya rasilimali zote zinazohitajika kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo. Huenda tusifahamu vya kutosha kuhusu athari za virusi hivyo kwa watoto au ni wangapi watakuwa wameathirika, lakini tunachofahamu ni kwamba ufuatiliaji wa karibu na kuzuia kusambaa zaidi ni muhimu sana kwani muda unatutupa mkono.”

Watu 6065 wameambukizwa virusi hivyo hadi sasa na idadi inaongezeka kwa kasi. Visa vingi viko China na kumekuwa na ripoti za watoto kuambukizwa pia.

UNICEF inawasiliana kwa karibu na mamlaka nchini China, ikiwemo wizara ya biashara na tume ya afya ya taifa, shirika la afya duniani WHO na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa ili kufuatilia hali na mahitaji wakati ugonjwa huo ukiendelea kusambaa.

UNICEF pia inafanyakazi kwa karibu na WHO na wadau wengine kuratibu hatua za pamoja za kudhibiti ugonjwa huo China na katika nchi zingine zilizoathirika.

Kwa mujibu wa WHO hadi kufikia leo nchini China jumla ya visa 5997 vimethibitishwa katika majimbo 31, na kati ya hivyo watu 1239 wako katika hali mbaya, 132 wamefariki dunia na wagonjwa 103 wametibiwa, kupona na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Na nje ya China visa 68 vimethibitishwa katika nchi 15.

Siku ya Jumatano, Shirika la Afya Duniani, WHO limethibitisha kwamba visa vya virusi vya  corona sasa vimesambaa na kuingia katika Falme za Kiarabu (UAE) ambapo kufikia leo virusi vya corona vimethibitishwa katika nchini 15 huku UAE ikiwa ni nchi ya kwanza ukanda wa Mashariki ya Kati kuathirika.

Kwa mujibu wa WHO watu wanne wa familia moja kutoka Wuhan, ambao walikuwa wamesafiri kwenda UAE mapema Januari, walilazwa hospitalini mnamo tarehe 25 na 27 Januari baada ya kugundulika kuwa na virusi vya corona.

Wakuu wa WHO, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa WHO,  Dkt.Tedros Ghebreyesus, wamekutana na Rais wa China Xi Jinping mnamo Jumanne ili kubadilishana taarifa juu ya mlipuko na kusisitiza kujitolea kwao kuudhibiti.

Baada ya kurejea  kutoka Uchina, Bwana Ghebreyesus amekaribisha mwaliko wa nchi hiyo kwa WHO kukusanyika na kuongoza timu ya wataalamu wa kimataifa ili kutathmini mlipuko wa virusi vya  corona, na kuunga mkono wenzao wa China.

Mkuu wa WHO ametangaza kwamba Kamati ya dharura ya WHO itakutana, kwa mara ya pili, Alhamisi,wiki hii  kuamua ikiwa mlipuko wa virusi vya corona ni dharura ya Afya ya Umma inayotia hofu ya kimataifa (PHEIC) au la.

Mkutano uliopita wa Kamati ulimalizika mnamo Januari 23 kwa uamuzi wa kutotangaza PHEIC, ingawa wanachama walikuwa wamegawanyika juu ya suala hilo.