Umasikini ulinifanya kuwinda wanyamapori lakini sasa nawalinda:Rabe

29 Januari 2020

Kutana na Jean Rabe amekuwa muwindani wa asili wa wanyamapori kwa maisha yake yote  lakini sasa baada ya kutambua umuhimu wa kulinda bayoanuai na mazingira ameamua kuwa mmoja wa wanamazingira na wahifadhi wa wanyamapori.

Katika Kijiji cha Marovovonana Kaskazini Mashariki mwa Madagascar wanayapori na misitu imesheheni, ni karibu kabisa na hifadhi ya asili ya Makira.

Muwindaji Jean Rabe akiwa na mbwa wake anasaka wanyama porini katika eneo hili ambalo uvuvi na wanyamapori ni sehemu kubwa ya chakula na maisha ya kila siku. Rabe anasema

(SAUTI YA RABE)

"Mbwa wangu wanawabaini kirahisi nguchiro, fungo na paka mwitu, pia siku za nyuma nimeshawahi kuwinda nguruwe pori, ni umasikini ambao umenisukuma kufanya hivyo. Nina mke na watoto wa kuwalisha “

Ingawa Rabe hawindi kila siku lakini fedha anazopata kutokana na kuuza nyama ya porini zinamsaidia na hata anaweza kuweka akiba kidogo.

Hata hivyo uwindaji huo na mabadiliko ya tabianchi vimeongeza tishio la bayoanuai katika jamii na hifadhi ya Makira hali iliyolifanya shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO likishiriiana na mpango wa udhibiti endelevu wa wanyama pori nchini Madagascar SWM kuchukua hatua ukiwashirikisha wadau wengine kuimarisha uhakika wa chakula, uhifadhi za matumizi endelevu ya wanyamapori kwa kutoa elimu kwa watu kama Rabe

(SAUTI YA RABE)

"Nnakula nyama ya porini pia japo sio sana, lakini pia anenda mtoni kuvua samaki, na siku hizi wanayamapori wameanza kuwa adimu  labda kwa sababu msitu unatoweka”

Baada ya kuelimishwa Rabe sasa amekuwa mjumbe wa timu ya doria inayofanya kazi kuhifadhi mbuga ya asili ya Makira na wanyamapori wake kupitia mradi unaotekelezwa na FAO na jamii ya hifadhi ya wanyamapori WCS kwa kuwapa wawindaji shughuli mbadala kama ufugaji. Rabe ameahidi  kwamba

(SAUTI YA RABE)

"Nitalinda misitu na taratibu nataka kuacha kabisa kuwinda  kwa sababu sasa nanufaika na ufugaji wa kuku. Na endapo tutasaidiwa mambo yatarejea kama yalivyokuwa zamani, na wanyama watajaza msitu tena na itakuwa vizuri sana kwa mustakbali wetu.”

Madagascar ni moja ya mataifa 12 barani Afrika, Caribbea na Pasifiki yanayoshiriki katika mradi huu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter