Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi dhidi ya wanaohusishwa na ISIL lazima izingatie katiba ya Iraq-Ripoti

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Jeanine Hennis-Plasschaert akitembelea Sinjar kwenye maadhimisho ya miaka mitano ya maovu yaliyotekelezwa na ISIL dhidi ya jamii ya Yazidi.
UNAMI/Sarmad As-Safy
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Jeanine Hennis-Plasschaert akitembelea Sinjar kwenye maadhimisho ya miaka mitano ya maovu yaliyotekelezwa na ISIL dhidi ya jamii ya Yazidi.

Kesi dhidi ya wanaohusishwa na ISIL lazima izingatie katiba ya Iraq-Ripoti

Haki za binadamu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binaadamu, OHCHR wamechapisha ripoti ya pamoja kuhusu hukumu chini ya sheria za Iraq za kigaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa OHCHR Jeremy Laurence amewaambia waandishi wa habari kwamba ripoti hiyo ni kutokana na ufuatiliaji wa hukumu 794 kwenye mahakama ya uhalifu ambako washtakiwa waliohusishwa na kundi la kigaidi la ISIL kuanzia Mei Mosi 2018 hadi Oktoba 2019 ambazo zilifanyika chini ya uungwaji mkono na baraza la majaji wa ngazi ya juu nchini Iraq.

Ripoti hiyo ya pamoja inatambua juhudi kubwa zilizochukuliwa za kuhakikisha uwajibikaji kwa makosa yaliyofanywa na wapiganaji wa ISIL, lakini hali ambayo inaongeza wasiwasi mkubwa ni juu ya mwenendo wa kesi kinyume na kuwaweka washtakiwa katika shida kubwa.

Bwana Laurence amesema ripoti, "ilikubali kwamba kesi za mahakama dhidi ya washtakiwa wa ISIL zimefanywa kwa utaratibu, zimepangwa vizuri, na majaji waliandaliwa mara kwa mara na nyaraka za uchunguzi."

Hata hivyo ripoti imebainisha kwamba "ukiukwaji wa viwango vya haki vya kesi umeweka washtakiwa katika shida kubwa ukilinganisha na upande wa mashtaka - kwa uwakilishi wa kisheria usio na ufanisi na uwezekano mdogo wa kutoa au kupinga ushahidi."

Pia inasema kwamba "kuegemea zaidi juu ya kukiri, na madai ya mara kwa mara ya kuteswa ambayo hayakushughulikiwa vizuri, wakati huo huo ukiukaji wa haki za binadamu, vyote  hivyo vinatia wasiwasi."

Ripoti pia imebaini kuwa mashtaka chini ya mfumo wa kisheria wa kupambana na ugaidi yalilenga zaidi ushirika wa kundi la kigaidi, bila kutofautisha kati ya wale walioshiriki kwenye ghasia, waliofanya uhalifu wa kimataifa, na wale ambao walijiunga na ISIL kwa ajili ya uhai wao na au kupitia kulazimishwa.

Taarifa ya msemaji wa OHCHR imemnukuu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet akisema, "mfumo sawa na wa haki ni kiungo muhimu katika njia ya maisha ya kidemokrasia, na ufunguo wa kujenga uaminifu na uhalali, na kukuza na kulinda haki za binadamu. . Wale wanaohusika na uhalifu ulioenea dhidi ya watu wa Iraqi lazima wawajibishwe, na ni muhimu kwamba waathirika waone kwamba haki inatendeka. Wakati huo huo, washtakiwa wana haki ya kushtakiwa kwa haki, na viwango hivi lazima vitekelezwe ipasavyo. "

Ripoti hiyo imewataka viongozi wa mahakama kufanya uchunguzi kamili wa kesi na vitendo vya hukumu kwa lengo la kuimarisha taratibu za haki za uhalifu, kulingana na katiba ya Iraq na majukumu ya serikali chini ya sheria za kimataifa.

Kwa upande wake Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Jeanine Hennis-Plasschaert amesema, "ulinzi salama wa kizuizini, mchakato unaofaa na majaribio ya haki sio tu unaonesha dhamira kwa ajili ya haki, ni muhimu katika kujnga stahamala. Ameongeza kwamba, 'Tunafahamu wazi kuwa baadhi ya malalamiko, ikiwemo mchakato wa kesi mbovu na unyanyasaji wa wafungwa, yamekuwa yakitumiwa na ISIL ili kuendeleza ajenda yake ya vurugu.”