Msaada umefika kwa maelfu ya manusura wa Kolom waliokimbilia mjini Abyei, Sudan Kusini

28 Januari 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na wahamiaji, IOM, hii leo mjini Abyei Sudan Kusini, wametoa taarifa ya kufikisha  misaada kwa manusura wa mashambulizi yaliyofanyika jumatano iliyopita katika mji wa Kolom, kilomita tisa kutoka mji wa Abyei.

Inaripotiwa kuwa idadi ya watoto isiyofahamika, walitekwaa katika tukio hilo. Mkuu wa IOM nchini Sudan Kusini Bwana Jean-Philippe Chauzy amesema, “tunasikitiswa sana na upotevu wa maisha ikiwa ni matokeo mabaya ya matukio ambayo yaamefanyika Kolom jumaa lililopita. Tunashirikiana na jamii hizi nainatia uchungu moyoni kuona kilichotokea.”

Tathimini ya haraka iliyofanywa tarehe 24 mwezi huu wa Januari ilionesha  kuwa takribani watu 4,000 walikimbilia katika mji wa Abyei. IOM Sudan Kusini na Sudan kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kimataifa wa misaada ya kibinadamu wameingilia kati kusaidia. Familia sabini zimepewa msaada wa kibinadamu wa haraka kama vile blanketi, mashuka na magodoro, madumu ya kutunzia maji, sabuni, sabuni na kama za mpira kwa ajili ya kutengeneza makazi ya muda.

Hata hivyo taarifa ya IOM imesema kuwa kuna watu takribani 3,600 katika maeneo mengine matano katika mji wa Abyei ambao bado wanahitaji msaada wa haraka.

Misaada mingine iliyotolewa ni pamoja na vyandarua na taa zinazotumia nishati ya jua huku IOM ikiendelea pia kusaidia kwa upande wa maji, usafi na kujisafi na pia wameanza kujenga vyoo vya dharura katika shule ya sekondari ya wavulana ya Abyei ambako inakadiriwa familia zipatazo 230 kutoka Kolom zimeweka makazi.

“Katika mazingira kama haya, tunafahamu kuwa watu wanakimbia katika uelekeo tofautitofauti. Kwa sasa hatua yetu ya haraaka imezifikia familia zilizokimbilia kituo cha Abyei tu lakini tunalenga kuzisaidia familia zote ambazo zimeathirika na janga hili na tahimini ya pamoja itatuonesha ni msaada gani unahitajika na wapi.” Ameeleza Asar Ul Haq, Mratibu wa proramu wa IOM Sudan Kusini.

Machafuko yamekuwa yakitokea kutokana na mgogoro wa muda mrefu kati ya jamii ya wakulima wanaojihusisha na kilimo wa kabila la Ngok Dinka na wale wa Misseryia ambao ni wafugaji.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud