Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima kuwe na uwajibikaji wa vifo vya mashambulizi ya anga Libya-UN

Hali baada ya mashambulizi ya Jumanne usiku dhidi ya kituo kinachoshikilia wakimbizi Tajoura, mashariki mwa Tripoli.
IOM/Moad Laswed
Hali baada ya mashambulizi ya Jumanne usiku dhidi ya kituo kinachoshikilia wakimbizi Tajoura, mashariki mwa Tripoli.

Lazima kuwe na uwajibikaji wa vifo vya mashambulizi ya anga Libya-UN

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umerejelea wito wake wa kuhakikisha kwamba  uchunguzi huru na wa kina unafanyika Libya dhidi ya mashambulizi ya Julai 2019 yaliyokatili maisha ya takribani wakimbizi na wahamiaji 53, na wahusika lazima wawajibishwe

Katika ripoti iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa kuhusu mashambulizi hayo ya anga kwenye kituo kinachoshikilia wakimbizi na wahamiaji cha Tajoura Libya wito umetolewa kwa pande zote katika mzozo kuhakikisha haki inatendeka, uchunguzi huo unafanyika na kila aliyehusika kwa ukiukwaji huo wa sheria za kimataifa anawajibishwa.

Shambulio hilo lilikuwa baya zaidi lililokatili maisha ya watu wengi kwa wakati mmoja tangu kuzuka upya kwa wimbi la machafuko nchini Libya.

Ripoti hiyo ya kurasa 13 iliyotolewa na, mpango wa Umoja wa Mataifa Libya UNSMIL na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa pia imetoa wito wa hatua za haraka kuzuia zahma kama hiyo kutokea tena katika mzozo wa Libya ambao kwa mwaka 2019 maisha ya watu 287 yalikatiliwa na raia wengine 369 walijeruhiwa, huku asilimia 60 ya vifo na majeruhi ni kutokana na mashambulizi ya anga.Ripoti hiyo imetokana na taarifa zilizokusanywa na ziara ya UNSMIL kwenye eneo la tukio, tathimini ya picha za video, ushahidi mwingine na mahojiano na manusura na mashahidi.

Ripoti hiyo imebaini kwamba mnamo Julai 2 lori lililokuwa na bomu lilipelekwa kituoni hapo kutoka kwenye karakana ya kukarabati magari ya  kikosi cha Daman ambacho ni kikundi chenye silaha mshirika wa serikali ya kitaifa ya Libya (GNA)

Shambulio la pili la anga lilitokea dakika 11 baadaye kwenye kituo cha Tajoura ambacho kinahifadhi wakimbizi na wahamiaji 616, na upande wa pili wa kituo hicho wa Hangar ambako kulikuwa na watu 21016 wanaume na wavulana 47 walipoteza maisha.

Ripoti pia inalkubaliana na uchunguzi wa awali wa Umoja wa Mataifa uliobaini kwamba mashambulizi hayo ya anga huenda yalifanywa na watu kutoka nje  japo imeeleza kwamba “Haiko bayana endapo mashambulizi haya ya anga yalifanyika chini ya amri ya jeshi la kitaifa la Libya ,LNA au yaliendeshwa na vikosi vya nje kwa msaada wa LNA”

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salamé amesema “Mashambulizi hayo ya Julai 2019 kwenye kituo cha Tajoura ni mfano halisi wa jinsi gani uwezo wa masuala ya anga umekuwa ni zahma halisi kwenye vita vya Libya, na hatari na athari kwa raia kutokana na watu kutoka nje kuingilia katika mzozo huo. Hi indio sababu ahadi iliyotolewa Berlin Januari 19 imetaka kukomesha uingiliaji huo na kuzingatia vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa”

Ripoti imetoa wito kwa pande zote hususan GNA na LNA pamoja n anchi zozote zinazosaidia upande wowote katika mzozo huo kufanya uchunguzi wa mashambulizi hayo kwa mantiki ya kuhakikisha uwajibikaji.

Akisistiza hilo Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema “Na wale watakaopatikana na hatia za uhalifu huo chini ya sheria za kimataifa ni lazima wawajibishwe.”

Ripoti pia imeitaka mamlaka nchini Libya kufunga vituo vyote vya wahamiaji na kuhakikisha kwamba wahamiaji na wakimbizi walioachiliwa kutoka kwenye vituo hivyo wanapatiwa ulinzi na msaada haraka iwezekanavyo.

Hadi kufikia mwisho wa Desemba 2019 watu 3186 walikuwa wanashikiliwa katika vituo mbalimbali vya wakimbizi na wahamiaji Libya katika mazingira magumu na hali mbaya. Na hivi sasa wakimbizi na wahamiaji 2000 wameelezwa kuwa karibu na eneo la mapigano mjini Tripoli na hivyo maisha yao kuwa hatarini.