Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID na serikali ya Sudan wakubaliana kurejesha mkakati wa pamoja wa usalama

Tarehe 3 Januari 2020 Jeremiah Mamabolo alipofika katika eneo la kambi iliyotelekezwa mjini El Geneina huko Darfur Magharibi kufuatia mapigano ya kijamii
UNAMID/Hamid Abdulsalam
Tarehe 3 Januari 2020 Jeremiah Mamabolo alipofika katika eneo la kambi iliyotelekezwa mjini El Geneina huko Darfur Magharibi kufuatia mapigano ya kijamii

UNAMID na serikali ya Sudan wakubaliana kurejesha mkakati wa pamoja wa usalama

Amani na Usalama

Ikiwa ni baada ya matukio ya hivi karibuni ya uporaji katika katika maeneo ya Umoja wa Mataifa huko Darfur Magharibi, Kusini na Kaskazini nchini Sudan, taarifa iliyotolewa na Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani jimboni Darfur, UNAMID hii leo mjini Zalingei Sudan imeeleza kuwa UNAMID imekubaliana na serikali ya Sudan kurejesha mkakati wa pamoja utakaoruhusu ushauri na maamuzi ya haraka kuhusu usalama.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mkutano huo umehusisha mwakilishi wa UNAMID anayehusika na ushirikiano na mashauriano Bwana Jeremiah Mamabolo pamoja na maafisa wa serikali ya Sudan.

Hatua hii pia ni mwendelezo wa mikutano kati ya Bwana Mamabolo aliyoifanya katika mji Mkuu wa Sudan, Khartoum na Waziri wa Ulinzi wa Sudan pamoja na Naibu Waziri wa masuala ya kimataifa mnamo tarehe 16 na 24 za mwezi huu Januari. Mikutano hiyo ilihusisha timu ya maafisa wa UNAMID, Wizara ya Ulinzi na maafisa wengine wa mamlaka za Sudan.

Bwana Mamabolo amenukuliwa akisema, “hii ni hatua muhimu kuelekea katika kuhakikisha usalama na ulinzi wa jamii, maafisa wa Umoja wa Mataifa na mali yanapotokea matukio kama la hivi karibuni la uporaji katika eneo la Kabkabiya.”

Bwana Mamabolo ameendelea kueleza faida za ushirikiano huo akitoa mfano, “mathalani katika tukio la Kabkabiya, baada ya Wizara ya mambo ya nje ya Sudan na vyombo vingine kufahamishwa, haraka walituma vikosi vyao katika eneo na kudhibiti kuendelea kwa uharibifu zaidi na pia uwezekano wa kuoteza maisha. Kikosi cha UNAMID kinachoundwa na askari kutoka Pakistan kilichoweka kambi Kabkabiya nao waliingia haraka ili kudhibiti hali. Ushirikiano huu unatakiwa kupongezwa na kufanyika tena katika siku za usoni wakti matukio kama haya yanapotokea.”

UNAMID imesema ina matumaini makubwa ya kurejea kwa ushirikiano wa pamoja wa usalama na imeeleza utayari wake wa kushiriki katika kufanikisha utekelezaji wake.