Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atembelea sinagogi, atoa heshima kwa waathirika wa mauaji ya maangamizi makuu

Picha ya maktaba ikimwonesha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres  akihutubia kwenye sinagogi la Park East jijini New York, Marekani (31 Oktoba 2018)
UN /Rick Bajornas
Picha ya maktaba ikimwonesha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kwenye sinagogi la Park East jijini New York, Marekani (31 Oktoba 2018)

Katibu Mkuu wa UN atembelea sinagogi, atoa heshima kwa waathirika wa mauaji ya maangamizi makuu

Haki za binadamu

Jumamosi ya leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametembelea sinagogi la Park East mjini New York Marekani ambako ametoa heshima kwa waathirika wa mauaji ya maangamizi makuu yaani Holocaust.

 

Hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye sinagogi imekuja wakati huu ili kuendana na siku ya kimataifa ya kukumbuka mauaji ya maangamizi makubwa ambayo inaadhimishwa kila tarehe 27 ya mwezi Januari kila mwaka. Katika siku hii mnamo mwaka 1945, kambi ya Auschwitz ambayo pia ilifahamika kama Auschwitz-Birkenau ilikombolewa na jeshi la Sovieti. Kambi hii ilikuwa inatumika kuwafanyia ukatili mkubwa wayahudi.

Akiwahutubia wale waliohudhuria katika sinagogi, Katibu Mkuu Guterres amesema, kuliko wakati mwingine wowote, mshikamano unahitaji hasa wakati huu ambao kuna ongezeko la chuki dhidi ya wayahudi na ongezeko la mashambulizi kwa wayahudi, ushirika wao na mali zao kote duniani ikiwemo New York.

Aidha ameeleza namna ambavyo unazi mamboleo unavyopata uungwaji mkono kutoka katika teknolojia ya sasa ya mawasiliano ya mitandao ya kijamii ambako chuki zinaenezwa na kueneza ubaguzi wa rangi na mambo mengine ambayo ni sumu kwa vijana wa umri mdogo.

Bwana Guterres amesihi, "wanadamu kutosahau kuhusu somo walilolipata kutokana na janga kubwa na mauaji ya maangamizi makuu na zaidi wakatae lugha za chuki."

Amewapinga vikali viongozi ambao wanataka umaarufu katika kutafuta mdaraka wanatumia lugha za chuki na kutengeneza mazingira ya hofu.

Amesisitiza elimu itumike ili kupambana na ujinga.